728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Sunday, October 16, 2016

  Wakosefu TBS watakiwa kujisalimisha, kuomba msamaha

  Serikali imewataka baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) walioshirikiana na wenzao wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kupitisha makontena zaidi ya 100 bila kukaguliwa na shirika hilo katika Bandari ya Dar es Salaam kujisalimisha haraka.

  Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw.Charles Mwijage alitoa agizo hilo mwishoni mwa juma wakati akizindua baraza la wafanyakazi wa Shirika hilo.“Nimeanza kukusanya orodha ya majina ya watu waliosaidia kupitisha makontena haya na nikija nayo hawatapona,” alisema.

  Aliwataka wote wanaojijua kuhusika kujisalimisha mapema na kutubu ili wasamehewe kabla haya hatua hiyo.Makontena hayo yalipitishwa katika bandari ya Dar es Salaam hivi karibuni bila ya kuthibitishwa na shirika hilo.

  Pia aliitaka TRA kuacha kutoa makontena bila ya shirika hilo kuthibitisha au kukagua ubora wa bidhaa zinazoingizwa hapa nchini sababu mwenye mamlaka hiyo ni TBS.

  Alisema watakaotubu kuwa walishiriki waseme walishiriki vipi na lini, walishirikiana na nani na wataje sehemu yalikopelekwa makontena hayo ili serikali iweze kusaidia kukomesha hali hiyo.Alisema anaamini kuwa waliofanya hivyo katika mamlaka hiyo walifanya kwa utashi wao bila ya ushiriki wa viongozi wao na kwamba sasa wakati umefika wa kukomesha tabia hiyo.

  Alilitaka baraza hilo kushirikiana na menejimenti na kuhakikisha matatizo yanayojitokeza yanapatiwa ufumbuzi kwa maslahi ya nchi na kwamba serikali itahakikisha inaongeza vitendea kazi na watumishi ili kufikia malengo ya shirika.

  Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Egid Mubofu, baraza hilo lina wajumbe 48 wanaotoka katika vitengo mbalimbali na litakaa kwa muda wa miaka mitano.“Baraza hili linaundwa kutokana na mkataba wa menejimenti na Chama cha Wafanyakazi (RAAWU),” alisema Dkt. Mubofu na kuongeza kuwa menejimenti itashirikiana na baraza kufanyakazi za shirika kwa tija.

  Alisema wafanyakazi wanatakiwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu katika majukumu yao ya kila siku.Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi (TBS), Prof. Mekanya Maboko alilitaka baraza hilo kufanya kazi kwa kushirikiana na menejimenti na bodi kuhakikisha shughuli za udhibiti wa ubora zinafanyika kwa ufanisi.

  “Bodi itaendelea kuisimamia menejimenti na kuishauri ifanye kazi kwa kuzingatia sera na sheria,” alisema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Wakosefu TBS watakiwa kujisalimisha, kuomba msamaha Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top