WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Tanzania ni miongoni mwa nchi saba Barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa
kasi zaidi hivyo amewakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta
mbalimbali ikiwemo ya viwanda.
Tanzania ni nchi ya pili kwa kasi ya
ukuaji wa uchumi Barani Afrika ambapo uchumi wake unakuwa kwa asilimia 7
ikiongozwa na Ivory Coast inayokua kwa asilimia 8.5, Senegal ya tatu (asilimia 6.6), D’jibout
ya nne (asilimia 6.5), Rwanda ya tano (asilimia 6.3), Kenya ya sita (asilimia 6.0)
na Msumbiji ya saba (asilimia 6.0).
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana
jioni (Alhamis, Oktoba 13, 2016) wakati akifungua kongamano la Jumuiya ya
Dawoodi Bohora lililohusu fursa za uwekezaji.
Amewakaribisha wanajumuia hiyo kuja
kuwekeza nchini. Kongamano hilo lilifanyika katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Mwalimu Nyerere.“Tanzania ina sera nzuri za kiuchumi ambazo zimesababisha uchumi wake
kuendelea kuwa imara kwa zaidi ya miongo miwili sasa. Naikaribisha jumuiya ya Bohora kuja kuwekeza
na kufanya biashara Tanzania,” alisema.
Waziri
Mkuu alisema makampuni yatakayowekeza nchini yatafaidika na uwepo wa malighafi za kutosha, sera nzuri uwekezaji pamoja na uhakika
wa usalama wa mali zitakazowekezwa nchini kwa sababu ya hali ya amani na
utulivu iliyoko nchini.
Alisema
licha ya Tanzania kuwa maeneo mazuri kwa ajili ya uwekezaji pia ina soko la
uhakika kwa sababu ya kuwa mwanachama wa jumuiya mbili ambazo ni Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zenye watu takriban milioni 600.
“Tanzania
ni kitovu cha biashara kwani inapakana na nchi nane ambazo kati yake nchi sita zinatumia bandari ya Dar
es Salaam kusafirisha mizigo yake. Mizigo hiyo husafirishwa kwa njia ya reli na
barabara,” alisema.
Nchi
zinazopakana na Tanzania ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia,
Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Zinazotumia bandari ya Dar es
Salaam ni Uganda, DRC, Rwanda, Burundi, Malawi na Zambia.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM.
IJUMAA, OKTOBA 14, 2016.
0 comments:
Post a Comment