728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Tuesday, October 25, 2016

  SMZ yakabidhiwa Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani kisiwani Pemba


  Na Masanja Mabula -Pemba

  SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imekabidhiwa rasmi Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, kutoka kwa Serikali ya Watu wa China baada ya Hospitali hiyo kukamilika kwa Ujenzi wake. Makabidhiano hayo yaliyofanyika katika hospitali hiyo Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba, yakishuhudiwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar.

  Akizungumza na wananchi Waziri wa Wizara ya Afya Zanzibar Mhe:Mahmoud Thabit Kombo, aliwataka wafanyakazi na wananchi kuithamini na kuitunza hospitali hiyo, ili vifaa vilivyomo viweze kudumu kwa muda mrefu. Alisema hospitali hiyo ni hospitali ya wananchi wa Mkoani, Chake Chake, Wete, Micheweni na Zanzibar kwa ujumla, hivyo jukumu la kulinda miundombinu yake iko mikononi mwa wananchiwenyewe.

  Kombo, alisema kwa sasa Hospitali ya Abdalla Mzee ni Hospitali ya kisasa zaidi kutokana na kuwemo kwa vifaa vya kisasa, pamoja na kuwa na hadhi ya kuliko hospitali ya Mnazimoja iliyopo Unguja. “Leo Serikali ya watu wa China imetukabidhi hospitali hii, na wametukabidhi ikiwa na vitu vingi na vipya vya kisasa zaidi, ambavyo wagonjwa wataweza kutibiwa hapa hapa kuliko kwenda nje ya Zanzibar”alisema.

  Akizungumiza juu ya madaktari, alisema tayari Serikali imeshaanza kulifanyika kazi suala hilo, ili kuona huduma bora zinapatikana kutokana na uwepo wa madaktari wa kutosha. Waziri Mahmoud, alisema Historia ya Zanzibar na China ni ya udugu, iliyoanza tokea mwaka 1972 baada ya timu ya kwanza ya Madaktari wa kichina kufika Zanzibar kuanza kujitolewa, hivyo ni vigumu udugu huo kuvunjika.

  Hata hivyo aliwatoa hofu wananchi wa Mkoani, juu ya Hospitali hiyo kuwa wanaweza kuitumia na kuhamia ili Rais wa Zanzibar atakapokuja kuizundua aweze kuona watu wanapatiw ahuduma hospitalini humo. Kwa upande wake Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Mhe:Xie Ziaowu, alisema mradi wa hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, ni moja ya kigezo cha ushirikiano baina ya Zanzibar na China katika kujali maisha ya kijamii.

  Alisema kujengwa kwa hospitali hiyo ni miongoni mwa ziara iliyofanywa na Mhe:Rais wa China Xi Jinping nchini Tanzania mwaka 2013 na kuonana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein naviongozi mbalimbali mara mbili. “China inathamini sana urafiki na Ushirikiano uliopo baina ya Zanzibar na Tanznaia na kutaka ushirikiano huo uweze kuendelea katika kukuza maisha ya watu nchini”alisema.


  Alisema Madaktari wa Kichina waliopo Zanzibar, wataendelea kuwepo ili kuhakikisha wanawahudumia wananchi wa Zanzibar katika utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi. Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Khamis Mussa Omar, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwani mashirikiano hayo ni ya muda mrefu tokea mwaka 1964 baada ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi leo. 

  Alisema tokea wakati huo Zanzibar na China imeendelea kuwa na urafiki na mashirikiano ya kudumu, ambapo china imesaidia Zanzibar mambo mengi yakiwemo Uchumi kwenye viwanda, kilimo, Afya, Maji, Elimu na michezo kwa upande wa Uwanja wa Mao.

  Kwa upande wa Miundombinu alisema, bado mradi mkubwa wa Uwanja wa Ndege wa Unguja jengo la abiria, ambalo linajengwa kwa sasa baada ya mashauriano kufikiwa, ujenzi wa bandari kubwa ya Mpiga duri kwa mashirikiano na China, pamoja na Mkonga wa mawasiliano.

  “Tunategemea mashirikiano haya yatazidi kuendelea baina ya Zanzibar na watu wa Jamhuri ya China, tunawashukuru sana kwa msaada ambao wamekuwa wakitupatia”alisema. Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dr Juma Malik Akili, aliwataka wananchi wa Pemba kuhakikisha wanavitunza na kuvithamini vifaa vilivyombo ndani ya hospitali hiyo.

  Alisema vifaa hivyo vitasaidia kutambua maradhi na kutibu maradhi kwa kutumia njia ya kisasa zaidi, hivyo ni jukumu la kila mtu kuhakikisha Hospitali hiyo na hadhi yake inaendelea kudumu daima. Naibu waziri wa Wizara ya Afya Zanzibar Mhe:Harusi Said Suleiman, alisema tukio hilo ni la kihistoria kutokana na ukubwa wa hospitali hiyo, huku akiwataka wananchi kuilinda miundombinu ya hospitali pamoja na vifaa.

  Nae ,Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba, Bakari Ali Bakari aliiomba Serikali kuruhusiwa kutumia jengo hilo kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi kwa sasa, pamoja na kupatiwa wafanyakazi wa kutosha kutokana na ukubwa wa jengo wenyewe, na bajeti kuongezwa ili kuweza kulihudumia jengo hilo.

  Ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani ulianza mwaka 2014 na kujengwa na kampuni ya Jiangsu Provincial Construction Group Co. Ltd kutoka China.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: SMZ yakabidhiwa Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani kisiwani Pemba Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top