728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Saturday, October 1, 2016

  SERIKALI KUTATUA CHANGAMOTO ZA MAJESHI:

  Na: Frank Shija, MAELEZO.

  SERIKALI imejipanga kuhakikisha inatatua na kumaliza kero zote zinazoyakabili majeshi yote nchini ikiwa ni jitihada zake za kuhakikisha kuna kuwa na ulinzi imara wa mipaka ya nchi na raia wake.

  Hayo yamebainishwa na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipokuwa akifunga mafunzo ya Kijeshi ya kutua ardhini kutoka ndani ya maji na kukomboa eneo lililokaliwa na adui (Amphibia Landing) ikiwa ni sehemu ya maadhmisho ya miaka 52 ya JWTZ, jana katika kijiji cha Baatini, Wilayani Bagamoyo.

  Rais Magufuli alisema kuwa anatambua kuwa zipo changamoto kadhaa ndani ya Majeshi yetu na kuwahakikishia kwamba atahakikisha zinatatuli kwani nia ya Serikali ni kufanya maboresho makubwa ya majeshi yote.

  Alizitaja moja ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na suala la Resheni ambapo suala hilo alikwisha toa maaagizo ya kubadili mfumo wa kuwa na Maduka yasiyolipa ushuru na kodi na badala yake Askari waongezewe fedha katika Resheni zao.

  Ametoa wito kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange kufikisha taarifa ya uchambuzi kuhusu Resheni hizo ili utaratibu wa kuanza kulipa kiwango kipya cha Resheni ufanyike.

  “Nataka Wanajeshi wote wafaidike kwa kupewa kiwango bora cha Resheni kuliko kuendelea na maduka yasiyolipa Kodi huku yakiwafaidisha watu wachache, fedha zitakazotoka na maduka hayo zitatumika kuongeza Reshini zenu na Serikali itaongeza pia”. Alisema Rais Magufuli.

  Aidha Rais Magufuli alitumia fursa hiyo kulipongeza Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa uimara waliounyesha katika mazoezi hayo ambapo alisema kuwa ameridhishwa na anaamini nchi iko salama.

  Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi amewapongeza makamanda wa Jeshi hilo kwa kufanikisha zoezi na kuongeza kuwa zoezi hilo siyo kwamba linaleta sifa kwa wanajeshi pekee bali naTaifa kwa ujumla.

  Waziri Mwinyi amewaomba wanajeshi kuendelea kufanya kazi kwa moyo wa uzalendo huku Serikali ikiendelea kushughulikia changamoto zao.

  Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange amefananisha Jeshi na Kompyuta ambazo zina sehemu ya Hardware na Software, ambapo alisema hardware ni vifaa na software ni rasilimali watu.

  Mkuu huyo wa Majeshi alimuhakikishia Mhe. Rais kuwa wanajeshi wetu ni imara, wanaipenda nchi yao na raia wake, wanajiamini na wako tayari muda wowote.

  “Mhe. Rais, nakuhakishia wanajeshi wetu wako imara sana, ni watiifu, waadilifu, wanaipenda nchi yao, na wanawapenda wananchi wenzao, tena wako kamili kwelikweli, nami najivunia kuwa kiongozi wao”. Alisema Mwamunyange.

  Awali akielezea mazoezi hayo Meja Patrick Sawala amesema zoezi hilo la pamoja la Amphibia Landing katika uwanja wa medani za vita limefanyika kwa lengo la kuonyesha namna wajashi wan chi yetu wako tayari kutekeleza majuku yao ya kulinda amani na mipaka ya nchi yake.

  Alisema kuwa suala kubwa katika zoezi hili ni namna ambavyo wanajeshi wanafanya kazi kwa kushirikiana wakati wa mapambano dhidi ya adui yao.

  Meja Sawala amesema kuwa zoezi hilo ambalo lilihusisha Vikosi vya Anga, Nchi kavu na Majini huku zana za kisasa za kivita zikitumika katika mazoezi hayo.

  Aliongeza kuwa kutokana na Jiografia ya nchi yetu ambayo inasehemu ya visiwa, zoezi hilo ni muhimu sana kwa ajili ya ulinzi na kujihami.

  Mbinu zilizotumika katika zoezi hilo zinafanana kwa kiasi kikubwa zile zilizotumiwa na Majeshi ya Umoja wa Afrika yakiongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mwaka 2008 kwa kushirikiana na jeshi la Shirikisho la Comoro kukikomboa kisiwa cha Anjouan kupitia operesheni ya`Demokrasia Comoro’

  JWTZ inaadhimisha miaka 52 tokea kuasisiwa kwake mnamo tarehe 1, Septemba, 1964 kufuatia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hali iliyopelekea kanzisha Jeshi jipya lenye sura ya muungano lililokuja kurithi Jeshi la Tanganyika Rifle lililokuwa upande wa Bara pekee.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: SERIKALI KUTATUA CHANGAMOTO ZA MAJESHI: Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top