728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Friday, October 14, 2016

  MCHANGO WA MWL.NYERERE KATIKA KUIMARISHA UHUSIANO WA TANZANIA NA NCHI ZA NJE

   
  Na. Immaculate Makilika- MAELEZO

  Kati ya mafanikio makubwa ya Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa Awamu ya Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kujenga umoja wa taifa kati ya watu wa makabila na dini tofauti, na hivyo kudumisha amani ya muda mrefu tofauti na hali ya nchi nyingi za jirani na hiyo imeifanya Tanzana iitwe “Kisiwa cha Amani”.

  Mwl. Nyerere amepanua wigo wa siasa ya Tanzania na mataifa ya nje ambapo ameimarisha uhusiano, ushirikiano na kuunga mkono vyama halisi vya Ukombozi wa Afrika kama vile FRELIMO ya Msumbiji, ZANU-PF ya Zimbabwe, ANC ya Afrika Kusini na MPLA ya Angola bila kusahau SWAPO ya Namibia pamoja na mataifa yaliyopo mabara ya Ulaya, Amerika na Asia.

  ‘Tukiimarisha kushirikiana kwetu, tukielewa kuwa vita vyao ni vita vyetu, tutaongeza sana nguvu zetu za kuleta ukombozi wa Afrika nzima’ anasema Mwl. Nyerere.

  Katika nukuu za Mwl. Nyerere, amewahi kusema “Uhuru wetu hauwezi kuwa kamili kama jirani zetu hawajapata uhuru.” Hii inadhihirisha jinsi gani muasisi huyu wa Tanzania alivyokuwa na dhamira ya dhati ya kushirikiana na mataifa mengine ya kiafrika.

  Katika Azimio la Arusha Mwl. Nyerere amewahi kusema Tanzania iko tayari kushirikiana kirafiki na nchi yoyote yenye nia njema bila kujali kama nchi hiyo ni ya upande wa Mashariki, kwa maana ya nchi zenye mlengo wa Kijamaa au Kikomunisti au Magharibi, zenye mwelekeo wa kibepari.

  Aidha, Mwl. Nyerere amesisitiza juu ya wajibu wa kuimarisha ushirikiano na kuungana mkono nchi za kimapinduzi za Afrika, kwa vile aliamini kuwa nchi zote zimo katika jahazi moja, yenye safari moja, akiwa na maana ya mazingira na hali za kufanana za nchi hizo.

  Katika kipindi cha Utawala wake wa Awamu ya Kwanza na hata baadae Mwl. Nyerere ameshiriki katika jitihada mbalimbali za kusaidia mataifa ya kiafrika kujipatia Uhuru wake, pamoja na kutatua migogoro iliyokuwepo katika nchi hizo. Amekuwa Mwenyekiti wa nchi zilizokuwa mstari wa mbele katika ukombozi wa Afrika pia amekuwa msuluhishi wa migogoro ya Burundi.

  Hali hiyo imesaidia Tanzania kuwa nchi yenye mahusino mema na nchi mbalimbali duniani bila kujali itikadi zao wala miongozo yao.

  Kutokana mchango na jitihada za Mwl. Nyerere, Tanzania imekua kivutio cha wageni wengi kutoka nje, kuanzia wanasiasa wa kimataifa na wasomi kutoka Marekani, Ulaya Magharibu na kwingineko.

  Wasomi hao wa Kimataifa kutoka maeneo mbalimbali walikuja kujionea na kufanya utafiti juu ya sera ya Tanzania siri iliyomwezesha Mwl. Nyerere kuiweka Tanzania katika ramani ya Dunia.

  “Pembuzi zao nyingi zilimwelezea Mwl. Nyerere kama “Roho ya Afrika na tumaini la wasomi, wanasiasa wa Afrika na Dunia nzima”, kila neno lake lina thamani kubwa, lenye kupimwa na kuchanganuliwa kwa makini na nchi za Magharibi na za Mashariki.

  Kitendo hicho cha jamii ya kimataifa kumfananisha Mwl. Nyerere na wafalme wa nchi za ustaarabu wa kwanza Duniani, kama Julius Ceasar, Suleimani na Richard wa II, ni uthibitisho tosha kwamba kipaji chake kilivutia wengi.

  Baadhi ya viongozi waliofurahishwa na uwezo wa Mwl. Nyerere ni pamoja na Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter ambaye mwaka 1977 alimsifia na kumwelezea Mwl. Nyerere kama “ Rais Mwandamizi, msomi, mwanafalsafa aliyetukuka na mwandishi mahiri”.

  Imewahi kuelezwa kuwa Rais Carter alichukua daftari (notebook) na kuandika kila kitu alichokuwa akisema Mwl. Nyerere na baadae gazeti moja nchini humo liliandika “Inapotokea Rais wa Taifa kubwa kumnukuu Rais wa Kiafrika” inaonesha ni jinsi gani busara ya Mwl. Nyerere ilivyoheshimika na mataifa makubwa.

  Mwl. Nyerere ameimarisha mahusiano baina ya nchi kadhaa na Tanzania katika harakati za ukombozi wa nchi hizo na uhusiano huo umezaa matunda ambayo ni msaada katika kukuza uchumi wa nchi husika pamoja na kuchangia maendeleo kwa kutoa fursa mbalimbali ikiwemo ajira, masuala ya kidiplomasia ama utatuzi wa migogoro, sekta za viwanda, afya, kilimo, elimu, teknolojia na biashara.

  Mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika ambazo bado zilikua zikikaliwa kimabavu na wakoloni katika nchi za Zimbabwe, Msumbiji , Angola, Namibia na Zimbabwe zimeimarisha uhusiano kati ya nchi hizo na Tanzania.

  Kuwapatia hifadhi salama vyama vya ukombozi vya mataifa, pamoja na rafiki wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Dr. Kenneth David Kaunda (aliyekuwa rais wa Zambia) ulisaidia jitihada za kuikomboa Afrika hususani Kusini mwa Afrika.

  Aidha, kupitia uhusiano uliojengwa wakati huo kati ya Mwl. Nyerere na Kenneth Kaunda ulifanikisha azma ya biashara ya nchi ya Zambia iliyokuwa ikiuza shaba kwa kiwango kikubwa katika nchi za China, Ujerumani na kwingineko kwa kujenga reli ya TAZARA kutokana na ufadhili wa Serikali ya China kutoka Dar es Salaam hadi ukanda wa shaba nchini Zambia.

  Reli hiyo ni mradi mkubwa wa kwanza kufanywa na China nje ya mipaka yao, lakini pia ndiyo reli bora zaidi kujengwa Duniani baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Mwl. Nyerere hakuishia Afrika pekee, ameimarisha mahusiano baina ya Tanzania na China ambayo kwa hakika yamekua yakileta faida kubwa kwa nchi zote mbili.

  Ni kutokana na mahusiano hayo mema kati ya Tanzania na China, ndio kumezaa matunda yaliyochangia juhudi zilizofanywa na Meya wa Mji wa Musoma Bw. Kisusura Malima na aliyekuwa Balozi Mdogo wa China nchini Li Xuhang alipokuwa mkoani Mara kuadhimisha miaka 50 ya Urafiki wa Tanzania na China.

  Juhudi hizo ni katika kuwaenzi wanamapinduzi, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na muasisi wa Taifa la China, Mao Zedong, kwa kuunganisha mji wa Musoma kilipo kijiji cha Butiama alipozaliwa Mwalimu na Jiji la Xiang Tan nyumbani kwa Mao mwasisi wa China.

  Miji hiyo inaungana kuifanya Butiama na Mara kuwa kivutio cha utalii, uwekezaji kibiashara na kitaaluma kwa kushirikiana Xiang Tan jiji lenye maendeleo makubwa.

  Mahusiano mazuri ya Mwl. Nyerere yalishamiri pia katika taasisi mbalimbali duniani, kwa mfano Robert Mac Namara, Rais wa zamani wa Benki ya dunia aliita Tanzania “kipenzi” chake cha Afrika.

  Naye, Gavana Jerry Brown wa Marekani alipotembelea Tanzania, alikaa juu ya magoti ya Mwl. Nyerere kwa kile alichosema “aweze kujifunza maajabu ya bara la Afrika kutoka kwa bingwa wa masuala ya Afrika na Dunia”.

  Ikumbukwe kuwa Mwl. Nyerere amekuwa na ushawishi mkubwa na alitoa wazo la kuunda mashirika mbalimbali yanayoziunganisha nchi za Afrika ikiwa ni hatua mojawapo ya kuelekea kuunda Afrika moja, hivyo mashirika kama vile SADC, ECOWAS, COMESA, EAC na kadhalika yaliundwa katika kufikia azma ya kuunganisha nchi za Afrika, na hivyo mashirika hayo yamekua yakiendelelea kufanya kazi hadi sasa.

  Ni dhahiri kuwa Tanzania imendelea kuaminika na kuwa kinara katika masuala ya diplomasia na amani duniani kote na kuifanya kuwa na mahusiano yaliyoimarika katika nchi mbalimbali . Na hiyo ikiwa ni juhudi zilizofanywa na Mwl. Nyerere wakati wa utawala wake na hata baada.

  Hakika mchango wake wa kukuza uhusiano wa Kimataifa na Tanzania utakumbukwa vizazi hadi vizazi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: MCHANGO WA MWL.NYERERE KATIKA KUIMARISHA UHUSIANO WA TANZANIA NA NCHI ZA NJE Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top