728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Monday, October 31, 2016

  Mambo 10 yaliyonigusa muswada wa habari.

  Na Joseph Sabinus, Nottingham University

  JUZI niliandika makala kuonesha kuwa kelele zinazoendelea kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari ukizitazama kwa undani utakubaliana nami kuwa ni matokeo ya kada isiyojiamini.

  Tasnia ya habari hapo nchini haijiamini na hili linaweza kuelezwa ama na miaka mingi ya kuhangaika kuwa na sheria yao huku zoezi hilo kila mara likikumbwa na sababu mbalimbali na kuahirishwa au kwa namna wanavyojenga hoja zao.

  Hata hivyo ukiziacha kelele hizo na kuanza kuusoma muswada huu kwa kina na kwa kutafakari makosa mengi yanayofanywa na vyombo vya habari popote duniani utakubaliana nami kuwa muswada huu, kama walivyosema pia Tanganyika Law Society na Twaweza, una mambo mengi mazuri na ni bora zaidi kuliko ile ya awali.

  Nilidhani wanahabari wangeshiriki vyema katika kuboresha yale maeneo yenye changamoto badala ya kuwaachia watu wa tasnia nyingine. Ni bahati mbaya wadau hawa wamechagua kuwa wanaharakati zaidi badala ya wanataaluma.  Binafsi baada ya kuusoma muswada nimebaini masuala makubwa yafuatayo katika hili. Naomba tushirikiane.  1. Sheria kutosajili mitandao

  Awali nilipomsoma Mbunge Zitto Kabwe nilistushwa kusikia kuwa sheria hii inalenga kubana hadi mitandao ya kijamii. Hata hivyo sheria haisomwi kama gazeti.

  Wakati Zitto alikuwa akisoma tafsiri ya neno “media” na kuona limejumuisha mpaka mitandao ya kijamii, ukweli ni kwamba ukiusoma muswada ule eneo ambalo sheria itahusika nalo kwa maana ya uratibu ni sekta iitwayo “print media”

  Kwa hiyo ni kujidanganya kusema sheria hii itasajili mitandao ya kijamii na vitu vinavyofanana na hivyo. Badala yake ukisoma kifungu cha 8(1) unauona ukweli huu.

  2. Habari ni taaluma

  Kwangu mimi, sijui kwa wanahabari wenyewe, muswada huu unaleta kwa mara ya kwanza mfumo madhubuti wa kuifanya sekta ya habari kuwa taaluma kamili na itakayoheshimika na kutambuliwa zaidi.

  Ukiutazama mfumo unaopendekezwa wa Bodi ya Ithibati katika ibara ya 10 utaiona “spirit” hii. Taaluma kuwa taaluma moja ya sifa ni hii. Lazima wanataaluma hiyo wawe na Bodi inayowasajili kwa viwango vilivyowekwa. Hata hivyo sijapata sababu kwa nini sifa hazijaanishwa kwa sasa.

  3. Bodi kumilikiwa na wanahabari

  Wakati nikiendelea kuusoma muswada huu pia nilipatwa na wasiwasi kuhusu kuundwa kwa Bodi hiyo ya Ithibati nikidhani ingejaa warasimu tunaowafahamu siku zote.

  Hata hivyo kama kuna jambo lingine la kuusifu muswada huu ni pamoja na muundo wa Bodi yake. Bodi itakuwa na wajumbe 7 na kati ya hao wanne (4) watakuwa ni wanataaluma ya habari akiwemo mwenyekiti wa Bodi.

  Haya ni mapinduzi makubwa katika uundaji wa Bodi za kitaaluma ambapo katika maeneo mengine ingezingatiwa tu uwakilishi labda wa jinsi, umri au taasisi. Katika hili tuwapongeze waliosanifu muundo wa Bodi hii.

  4. Bara Huru lenye meno

  Hapa nianze kwa kusema muswada huu umechelewa sana na hakuna hoja wala haja ya kusubiri tena. Wananchi wanahitaji kuhudumiwa na sekta bora zaidi ya habari na kila mmoja wetu anajua umuhimu huu.

  Ukisoma kifungu cha 23 na kuangalia majukumu yale ya Baraza Huru la Habari utakubaliana nami kuwa tunahitaji Baraza hili Huru kuliko wakati wowote. Hilo Baraza linalotajwa kuwepo ni NGO tu na Serikali yoyote duniani haiwezi kuendeshwa na NGO.

  Baraza linaloundwa humu nimeona litakuwa na uhuru na haki ya kutunga kanuni za maadili za wanahabari na kuhakikisha wenyewe wanazielewa katika kuwasimamia kwenye kazi zao. Hii ni muhimu sana.

  Ukienda Mahakamani inachukua miaka. Ukienda MCT ya sasa hata wakitoa uamuzi chombo cha habari kinakuwa na uhuru wa kuukataa au kuukubali uamuzi huo. Baraza hili kwa kuwa limeanzishwa kisheria na lina nguvu za kisheria litakuwa na uwezo wa kusimamia hata utekelezaji wa hukumu zake.

  5. Wanahabari kutunga kanuni zao

  Katika hili niseme tu kwamba kama kuna jambo wanahabari wamekuwa wakilikosa kwa muda sasa ni kwanza kuwa na chombo kimoja kinachowaunganisha bila kuwabagua zaidi ya wao tu kuwa wanahabari.

  Katika Baraza linaloanzishwa nimeona vifungu kuwa litakuwa na kazi nyingine muhimu na ya kipekee (exclussive rights) ya kuandaa kanuni za maadili (media code of ethics). Hii ni muhimu kwa sababu badala ya kutungiwa na watu wengine ni wanahabari wenyewe watakaozitunga kwa sababu pia wanafahamu vyema kazi yao.

  6. Kamati ya malalamiko

  Kumekuwa na fikra miongoni mwa watu kuwa kuipata haki mahakamani ni gharama kubwa sana na inayochukua muda mrefu. Katikati ya keleleza za baadhi ya watu kuwa sheria hii haina jema, ni muhimu kuona umuhimu wa kifungu hiki.

  Kwa kuanzishwa Kamati ya Malalamiko chini ya Baraza Huru la Habari, sasa wananchi watapata pa kulalamikia na tena penye meno. Lazima tukubali kuwa ama kwa ajenda fulani au makosa ya kibinadamu, vyombo vya habari nchini vinawakosea sana watu binafsi au taasisi.

  Naamini ni vyema kuwapa wahusika mahala pa kulalamika kwa sababu kwenda Mahakamani ni suala ambalo kila mmoja, kwa sababu tulizokwishaeleza, asingependa kulichagua. Kamati hii basi ikiundwa itoe uamuzi kwa haraka na iwe madhubuti.

  7. Bima ya Afya

  Mwezi Novemba mwaka jana nilirejea nchini kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka. Katika pita pita zangu jijini Dar es Salaam nilikutana na matukio mawili ya wanahabari kuchangiwa na wenzao.

  Nilipofuatilia suala hili nikaambiwa kuwa wanahabari hao hawakuwa na bima na walipopatwa na maradhi ya muda mrefu ikawalazimu kuishi na kupata tiba kupitia michango ya kujitolea ya wanataaluma wenzao.

  Wapo pia waandishi ambao hadi sasa wako hai lakini wanaishi kwa kutegemea misaada ya ndugu na jamaa kwa ajili ya kupata huduma za afya. Nauona muswada huu unakuja kuwakomboa wanahabari. Ni muswada unaokuja kuhakikisha kuwa si tu wanataaluma hii wanafanya kazi zao kwa ufasaha lakini pia waweze kupata haki yao ya matibabu na kuwekewa hifadhi ya jamii.

  Iliniuma na leo tunapoona katika kifungu cha 58 cha muswada huu kuna ulazima kwa wamiliki wa vyombo vya habari kuwakatia bima watu wao, inashangaza kuona wapo wanahabari ambao wanadai muswada huu haufai na kutaka urejeshwe nyuma.

  8. Haki za watu

  Ukisoma Tamko la Haki za Binadamu la 1948 utaona msingi wa haki kuwa umebebwa katika dhana ya haki ya mtu mmoja hukoma pale utekelezaji wa haki hiyo unapoingilia uhuru au haki ya mtu mwingine.

  Nimeviona vifungu kadhaa vya muswada huu vikiwa na mlengo huu wa kuhakikisha wakati, kwa mfano, haki ya wanahabari kukusanya na kusambaza habari ikiwa ni muhimu, pia ziko haki za watu wengine zinazopaswa kulindwa na wanahabari.

  Kifungu cha 32 katika hili kwa mfano kinaainisha au kukataza waandishi kuchapisha kashifa na kuwashushia watu wengine hadhi zao bila sababu (wawe hai au wamekufa). Hii ni muhimu sana.

  9. Usalama wa Nchi

  Nikikumbuka jinsi vyombo vya habari vilivyochangia katika machafuko katika nchi mbalimbali duniani hasa Rwanda (1994) na Kenya (2007) nashawishika kuchekelea ninapousoma muswada huu.

  Ukiacha vifungu vinavyoainisha uchochezi, nimeguswa zaidi na kifungu cha 55 cha Sheria kinapompa mamlaka Waziri akijiridhisha kuwa kuna suala linalokwenda kukiuka usalama wa nchi basi achukue hatua haraka.

  Wanaharakati hupinga vifungu kama hivi kwa hoja za juu juu tu za kutokuwaamini viongozi wanaoweza kupewa madaraka hayo, lakini uhalisi kwamba mambo haya yameshatokea na kwamba zipo nchi zimeshawahi kuingia katika umwagaji wa damu kwa vyombo vya habari kuachwa huru watakavyo, mtu hawezi kubeza kuwekwa kwa vifungu kama hivi.

  Lipo pia kosa la uchochezi ambalo wengi, bila kulitafakari, wanapiga kelele zilizokosa tafakuri. Unawezaje kuwaacha watu watumie vyombo vya habari kuchochea vurugu, kuhamaisha uasi na machafuko katika nchi? Kwangu mimi makosa kama haya ni muhimu kwa usalama wa nchi na ni juu ya kila mmoja kutekeleza sheria.

  10. Kufutwa sheria ya Magazeti

  Mimi nikiwa hapo nyumbani kwa miaka mingi nimekisikia kilio cha wadau dhidi ya Sheria ya Magazeti, 1976. Sheria hii tumekua nayo, tumeishi nayo na tulianza kuzeeka nayo lakini kila mwanataaluma akijua haikuwa sheria nzuri.

  Kwamba leo inafutwa ni faraja kwa tasnia na nilidhani wenzetu wengine badala ya kulaani jambo hili wangeungana nasi kulishangilia. Kwangu, kama kuna jambo jingine kubwa kwa wanatasnia kulishangilia ni kufutwa kwa sheria hii ambayo wengine walifikia hatua ya kuiita “ya kikatili.”

  Wakati nikiamini wabunge watakuwa wamefanyiakazi changamoto nyingine na kuuboresha muswada katika maeneo machache kama vile kukamatwa mitambo kabla ya uamuzi wa mahakama na kuainishwa viwango vya taaluma, niwaase wanahabri nchi kuwa katika ulimwengu wa utatuzi wa migogoro; mazungumzo ni muhimu.

  Ni bahati mbaya kwamba katika hili walichagua kutozungumza na Kamati ya Bunge na wakasusia na hatimaye muswada huu ukipita utawahusu hata kama wao hawakushiriki kuutunga.

  *Mwandishi wa makala haya amejitambulisha kuwa ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu (PhD) kwenye Chuo Kikuu cha Nottingham, Uingereza.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Mambo 10 yaliyonigusa muswada wa habari. Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top