728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Wednesday, October 12, 2016

  MAKALA YA MWALIMU NYERERE- NA WANANCHI WA KIJIJI CHA MWANGOZO

  Judith Mhina - Maelezo

  Msingi wa Umoja, Upendo Amani na Mshikamano ni vijiji vya ujamaa, hayo yamesemwa na muasisi wa kijiji cha Ujamaa cha Mwongozo Bw Cyprian Francis Komba, wakati akifanya mahijiano na Idara ya Habari Maelezo kijijini hapo. Kijiji cha Muongozo kipo Kata ya Somangila Wilaya ya Kigamboni.

  Mzee Komba anasema Vijiji vya Ujamaa vimesaidia kwa asilimia kubwa kujenga umoja, upendo, amani na mshikamano hapa Tanzania, pamoja na sera ya Mwalimu, ya elimu ya kuwaweka katika shule moja wanafunzi wa Tanzania kutoka maeneo mbalimbali kwenda kusoma kwenye maeneo ambayo sio ya wazazi wao kwa asili.

  Akitoa mfano Mzee Komba anasema, aliona wanafunzi wengi wa Songea walikuwa wanapelekwa shule za sekondari mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Dodoma, ambapo Songea katika shule ya wasichana Songea walikuwa wanakuja wanafunzi kutoka Kagera, Tanga, Kilimanjaro, Mbeya na sehemu nyingine za Tanzania. Hii ina maana wanafunzi hao walijifunza mambo mengi kutoka Mkoa wa Ruvuma na pia kati yao wenyewe walifahamiana kwa karibu miaka minne kwa uzuri na kujenga misingi ya Umoja, Upendo, Amani na Mshikamano kama familia moja.

  Aidha, aliongeza kuwa Jeshi la Kujenga Taifa pia lina mchango mkubwa katika kuimarisha na kuijenga hali ya Umoja, Upendo Amani na Mshikamano. Katika kambi mbalimbali Tanzania vijana walikuwa wanakutana kutoka maeneo tofauti hii ilipunguza sana kuondoa tofauti za vijana na kuwafanya wajione ni watanzania zaidi kuliko makabila yao. Unayeishi naye kwa muda mrefu unajenga tabia au hisia ya kuwa ndio ndugu yako anayeweza kushirikiana na wewe kwa shida na raha. Alimalizia kwa kusisistiza yote hayo matatu ni ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.


  Mzee Cyprian Francis Komba au Jomo, Muazilishi wa Kijiji cha Ujamaa Mwongozo na Mmoja wa vijana 75 wa Jumuia ya Vijana ya TANU - TANU Youth League

  Akieleza historia ya kijiji hicho alisema; Kijiji cha Ujamaa cha Muongonzo kilianzishwa mwaka 1975, ambapo wakati huo Mzee Komba na vijana wenzake 75 ambao walikuwa ni wahamasishaji wa chama cha Tanganyika African National Union- TANU, chini ya mwamvuli wa Jumuia ya Vijana ya TANU au TANU Youth League, walikubaliana na Chama kuanzisha makazi rasmi mara baada ya uhuru. Ndipo Chama kikatafuta maeneo mawili yaani Kerege Bagamoyo na Mbwa Maji Gezaulole, kundi la Mzee Komba lilifika eneo la Mbwa Maji – Gezaulole tarehe 10 Machi 1963.

  Vijana hao 75 baadaye walihamia katika mradi wa scheme kwa ajili ya kuanzisha makazi ya kambi ya vijana tarehe 10 Oktoba mwaka 1963,wakiwa pamoja na Mwalimu Nyerere ambaye alizindua utaratibu wa kijiji hicho ambao ulijulikana kwa jina la scheme ,kwa kupanda mti wa Mvule, ambo upo hadi leo.

  Vijana hao 75, walitoka katika makabila mbalimbali ya Tanzania. Hivyo, Sera ya Ujamaa na kujitegemea ilianza kutekelezwa mwaka 1975 kwa sheria ya vijiji vya Ujamaa, ndipo kijiji cha Muongozo kikatangazwa rasmi kuwa kijiji cha Ujamaa.

  Komba anaongeza kwa kusema, hata ungefika kijiji hapo wakati huo, usingeamini kwamba wanakijiji hao sio ndugu wala hawatoki kabila moja. Tulikuwa tunapendana sana na kushirikiana kwa kila hali. Sasa hapo umoja, upendo, amani na mshikamano ndio ulijengwa na ndio chimbuko la amani la nchi hii.

  Mwalimu Nyerere mara baada ya kuanzisha kijiji cha Ujamaa alipima ardhi yote ya kijiji na kutenga eneo la shule , zahanati, mradi wa maji, shamba la mikorosho hekari 37, mpunga 15, mahindi 10 na pamba heka saba. Aidha kila mwanakijiji alikuwa na robo heka ya kulima zao la chakula , ambapo wengi tulilima mahindi; amesema Komba

  Kijiji kilikuwa na utaratibu wa kufanya kazi kwa msaragambo au pamoja katika mashamba ya kijiji na mashamba binafsi ya kila familia. Huu ni utekelezaji wa mpango wa Uhuru na Kazi. Kama umesoma kitabu cha Azimio la Arusha kipengele cha kujitegemea sehemu ya tatu; kufanya kazi kwa bidii na maarifa ni sehemu ya utekelezaji wa Azimio la Arusha.

  Mzee Komba aliongeza kwa kusema, vijiji vimetufundisha suala zima la kujitegemea, unaona zahanati hii inatumika hadi leo ni matunda ya kujitegemea, tuna shule ya msingi pia tulijenga sisi wenyewe kwa umoja wetu. Pia tulikuwa na mradi wa maji kila nyumba ilipata maji kulikuwa na mambomba yalisambazwa na wataalamu wa maji lakini mitaro tulichimba wenyewe na kufukia. Nasikitika kukuambia sasa hivi mradi wa maji haupo maana wasiojua maana ya vijiji wamengoa mabomba na kuuza chuma chakavu mara baada ya mashine ya kusukumia maji kuharibika.

  Mpaka sasa katika kijiji hiki wale vijana wote 75 wa TANU Youth League tumebaki vijana watatu tu, yaani mimi Mzee Mbwana na mke wake, wenzetu wote wameshatangulia mbele za haki. Pia ipo kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ambaye alipanda mti wa Mvule katika kuanzisha scheme ya kijiji chetu mwaka 1963.


  Mti wa Mvule alioupanda Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tarehe 10 Oktoba mwaka 1963, Mradi wa Scheme katika Kijiji cha Mwongozo Wilaya ya Kigamboni.

  Mzee Komba ameendelea kusema, Mwalimu Nyerere Mungu amlaze mahala pema peponi, alikuwa rafiki yangu sana, na hata vijiji vya ujamaa vilipovunjika, alikuwa anakuja kututembelea mara kwa mara na kuona maendeleo yetu ya zao la korosho, mpunga, mahindi na pamba. Ila kwa sasa sina nguvu tena ya kulima japo ningependa kufanya hivyo, eneo la kijiji limepungua sana baada ya familia kuongezeka na eneo kubwa kupewa Serikali ya Kata.

  Mimi mpaka sasa nimekuwa nikiwaasa vijana wapende kufanya kazi hasa kilimo maana kina manufaa kuliko kila kijana kufanya biashara ndogondogo sina hakika kama wanafaidika sana. Kama umepita katika eneo la shamba la kijiji imebaki mikorosho tu, ambayo hailimiwi iko kama pori., hali hii mimi binafsi hainifurahishi.

  Ombi langu naomba unipelekee salamu kwa Wazee wa Chama cha Mapinduzi pale Ofisi za Chama Lumumba, na hasa zimfikie Rais Dkt. John Pombe Magufuli mwambie kuna wazee wa Chama cha Mapinduzi wako Kigamboni, kijiji cha Mwangozo aje atuone. Zamani nilikuwa nina nguvu naweza kwenda Lumumba, lakini tangu Mwalimu Nyerere alipotangulia mbele za haki, sijaweza kwenda na uzee huu ni ngumu. Hakika Mwalimu, alikuwa anatupenda sana.

  Bw Komba ambaye kwa sasa ni mzee wa miaka 94 alizaliwa Mkoa wa Ruvuma wilaya ya Songea tarehe 02 mwezi Machi mwaka 1923. Mwaka 1960, alijiunga na Jumuia ya vijana ya chama cha Tanganyika African National Union - TANU na 1961 alihamia Mkoa wa Dar-es-Salaam kwa ajili ya kuhamasisha watanganyika kujiunga na chama cha TANU, kampeni ya nyumba kwa nyumba.


  Bibi Fatuma Mohammed Mke wa Mzee Abraham Mbwana Muazilishi wa Kijiji cha Ujamaa Mwangozo

  Wanachama wengine wa TANU Youth League ni Bibi Fatma Mohammed ambaye alisema mimi namkumbuka sana Mwalimu Nyerere nina hakika angekuwa hai angekuja kututembelea na kutujulia hali maana alikuwa mwenzetu, ndiye aliyetuleta hapa. Mimi kwetu ni Msanga Wilaya ya Kisarawe nilikuja hapa nilipoelewa. Mume wangu Mzee Mbwana yeye alizaliwa maeneo ya Mbwa Maji na kukulia hapa hapa.

  Nilipoolewa nimemkuta Mzee Mbwana ni Mwanachama wa TANU Youth Legue na mmoja wa vijana 75 wa Mwalimu Nyerere. Kwa kweli sisi tulikuwa tunafanya kazi kweli kweli sio vijana wa siku hizi hawapendi kazi za uzalishaji za kilimo. Hapa Mwongozo bado kuna eneo kubwa tu la kilimo lakini hawataki hata kusikia. Nadhani tumewalea watoto wetu vibaya.

  Wakati wetu sisi tuliishi kwa umoja, amani na upendo mkubwa kati ya wanakijiji, hakika amani ilikuwepo, tuliishi kama ndugu, sasa maisha yamebadilika sana sijui serikali itafanyaje katika kudumisha hali iliyokuwepo siku za nyuma. Kila mmoja alikuwa na kazi ya kufanya kwa bidii, hakukuwa na wazururaji wala wezi . tunaomba Mwenyezi Mungu atunusuru na hali hiyo, alimalizia.

  Ndugu muandishi Upendo aliotuachia Mwalimu Nyerere ni wa ajabu mpaka leo hii wale waasisi ni ndugu wala huwezi kujua kama Mzee Komba sio Mzaramu. Mimi namuona kama shemeji yangu aliyezaliwa na Mbwana. Hakika Mwalimu tutamkumbuka sana sana siwezi kumsahau kamwe. Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani. Alimalizia bibi Fatma.  Mzee Cyprian Francis Komba Muanzilishi wa Kijiji cha Ujamaa Mwongozo  Mzee Abraham Mbwana Muanzilishi wa Kijiji cha Ujamaa Mwongozo na Mmoja wa vijana 75 wa TANU Youth League

  Mzee Abrahmani Mbwana alitoa shukurani kwa kuwa wameweza kupata mtu wa kutuuliza mambo ya Ujamaa. Yalikuwa mambo mazuri sana na wakati ule ukilima kidogo tu unavuna mavuno mengi mazuri, hakika hatukuwa na shida ya chakula hata kidogo.

  Namshukuru Mwenyezi Mungu nimeweza kuweka vibanda vyangu hapa kama unavyoona yote hii ni kazi ya mikono yangu na ardhi niliyouza baada ya kijiji kusimama. Kwa bahati mbaya Mzee Mbwana na mke wake hawakumbuki tarehe wala mwaka waliozaliwa ila ni marika na Mzee Komba.

  Wanakijiji hawa hawako mbali na mawazo ya Bibi Selma James ambaye ni Mwanaharakati wa kupinga ukatili dhidi ya Jinsia hasa wanawake anayeishi Mji wa New York aliyepata fursa ya kuelezea Azimio la Arusha na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Kongamano la Kimataifa la kutetea haki za wanawake London 2014. Bibi Selma alikuwa anunukuu vifungu vya Baba wa Taifa katika kufafanua jinsi alivyopigania haki za wanawake na watu waishio vijijini Tanzania. Aidha, Bibi Selma James alisema anashangazwa na amani aliyoikuta Tanzania amani kila mahali na kuahidi kufanya utafiti juu ya jambo hilo.

  Katika makala hii Mzee Cyprian Francis Komba amesema chanzo cha Umoja, Amani, Upendo na Mshikamano ni Vijiji vya Ujamaa maana waliishi kwa usawa bila kubaguana. Sera ya elimu ya kuchanganya wanafunzi kutoka kila pembe ya Tanzania, wanafunzi waliokuwa wanahitimu katika vyuo mbalimbali na wahitimu wa kidato cha sita, kwenda mwaka mmoja, katika kambi za Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: MAKALA YA MWALIMU NYERERE- NA WANANCHI WA KIJIJI CHA MWANGOZO Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top