728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Wednesday, October 19, 2016

  JELA KWA KUGHUSHI HUDUMA ZA NHIF

  Mkazi wa Dar es Salaam Bw. Michael Francis baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya shilingi milioni moja kwa kosa la udanganyifu katika huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
  Mshitakiwa wa Pili na wa Tatu wakiwa chini ya ulinzi baada ya kutiwa hatiani na kuhumiwa kifungo cha miaka miwili jela.
  Mshitakiwa Bw. Francis muda mfupi baada ya kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya udanganyifu.
  Mshitakiwa Bw. Godfrey Nyika ambaye ndiye kitambulisho chake cha matibabu kilitumiwa isivyo halali na BW. Francis baada ya hukumu.

  …………………………………………………………

  Na Grace Michael

  MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kinondoni imewahukumu wakazi wawili wa Mkoa wa Dar es Salaam kifungo cha miaka miwili jela au faini ya shilingi Milioni moja kwa makosa ya kujipatia huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa njia za udanganyifu.

  Hukumu hiyo imetolewa leo mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mwandamizi Bweguge Obadia ambaye alisema kuwa ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashitaka umeithibitishia mahakama pasipo shaka ya aina yoyote kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo.

  Waliohukumiwa kifungo hicho ni pamoja na Bw. Michael Francis na Bw. Godfrey Nyika ambao ni washitakiwa wa pili na wa tatu huku mshitakiwa wa kwanza Bw. Rashid Kidumule akiaachiwa huru baada ya kuthibitika kutotenda kosa hilo.

  Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mwandamizi Bw. Obadia alisema kuwa hakuna shaka yoyote juu ya washitakiwa hao kutenda makosa ya kujiwakilisha katika duka la dawa la Nakiete kwa lengo la kujipatia huduma ya dawa kwa kutumia kitambulisho cha matibabu cha mshitakiwa wa tatu ambaye ni Bw. Nyika.

  “Ushahidi wa mashahidi wa mashitaka unathibitisha bila kuacha shaka yoyote kuwa mshitakiwa wa pili Bw. Francis alijiwakilisha dukani kwa lengo la kupata dawa kwa kutumia kadi isiyo yakwake na hakuna shaka kuwa mshitakiwa wa tatu ambaye ndiye mwenye kadi alimpatia kadi hiyo mshitakiwa wa pili hivyo kwa ushahidi huu Mahakama inawatia hatiani,”anasema Hakimu Mkazi Bw. Obadia.

  Alisema kuwa Mahakama hiyo imezingatia makosa waliyoshitakiwa nayo washitakiwa hao pamoja na uhusika wao katika kutenda makosa hayo. Kutokana na hali hiyo, Mahakama ilimhukumu Bw. Francis kifungo cha miaka miwili jela au faini ya shilingi milioni moja huku mshitakiwa Bw. Nyika akihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja au faini ya shilingi laki tano.

  Washitakiwa hao walitenda makosa hayo ya kujiwakilisha kwa lengo la kujipatia huduma mwaka 2014 ambapo kesi hiyo imehitishwa kwa wao kukutwa na hatia na kuhukumiwa adhabu hiyo.

  Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya umekuwa ukitahadharisha wanachama wake juu ya matumizi ya vitambulisho vyao vya matibabu kwa kuonya kufanya udanganyifu wa aina yoyote kwenye huduma zake.

  Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bw. Bernard Konga amesema Mfuko utaendelea kuchukua hatua stahili kwa wanachama wasio waaminifu ambao watajihusisha na udanganyifu wa aina yoyote.

  “Nitoe tu tahadhari kwa wanachama na watoa huduma wote kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuulinda Mfuko kwa kuhakikisha huduma anayoitoa au kuipata iko katika njia sahihi, Mfuko hautakuwa tayari kufumba macho kwa wanaojihusisha na udanganyifu au kuhujumu Mfuko kwa namna yoyote,” alisema Bw. Konga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: JELA KWA KUGHUSHI HUDUMA ZA NHIF Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top