728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Thursday, October 6, 2016

  AGIZO LA DC ZANZIBAR LAGONGA UKUTA,MADAKTARI WAKWAMA KUHAMIA KIJIJINI

  Na Salum Vuai, MAELEZO

  AGIZO lililotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kati Mashavu Sukwa Said kumtaka daktari na wauguzi wa kituo cha afya Unguja Ukuu kuhamia katika nyumba zilizoko kijijini humo limegonga ukuta.

  Mwandishi wa habari hizi aliyefanya ziara kijijini hapo, aligundua kuwa nyumba hizo mbili ambazo zimekamilika kiujenzi, hazina samani wala vifaa vyengine vya ndani kuwawezesha watendaji hao kuhamia kama walivyoagizwa na kiongozi huyo.

  Kwa mara ya mwisho, Mkuu huyo wa Wilaya alitoa agizo hilo Septemba 9, 2016 wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa mabaraza ya vijana kwa shehia za Unguja Ukuu, akitaka ndani ya wiki moja, wafanyakazi hao wawe wameshahamia katika nyumba hizo.

  Wakizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina yao, baadhi ya wauguzi walisema kuhamia katika nyumba hizo sio tatizo kwao kama zitakuwa na vifaa ikiwemo vitanda, makabati na vitu vyengine.

  “Sisi tuko hapa kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi na tuko tayari kwa hilo lakini iko haja kwa kituo hichi kuwekewa mazingira mazuri, maana hakuna anayeweza kulala au kuweka vitu vyake sakafuni,” walisema.

  Aidha walisema, ingawa wanatakiwa kufungua kituo kwa saa 24 kwa ajili ya kutoa huduma za uzazi, wanashindwa kufanya hivyo kutokana na ukosefu wa dawa za msingi kwa ajili ya mama wajawazito kabla na wakati wa kujifungua.

  Alipoulizwa Mkurugenzi Kinga katika Wizara ya Afya Dk. Fadhil Mohammed Abdalla, alikiri kuwa nyumba hizo kwa sasa haziwezi kukalika kwa kuwa hazina samani ingawa ujenzi wake umekamilika kwa maeneo yote.

  Alisema kwa jumla kuna nyumba 13 hapa Unguja na tisa Pemba zilizojengwa sambamba na vituo vya afya katika maeneo mbalimbali mijini na vijijini kupitia mradi uliofadhiliwa na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Denmark (DANIDA), lakini haukujumuisha samani.

  Tatizo jengine, alitaja kuwa ni uhaba wa wafanyakazi, akisema katika hali ya kawaida, kila kituo kinahitaji watendaji wanane watakaofanya kazi kwa kupishana.

  Alisema daktari na muuguzi ni binadamu ambao hawawezi kutumika kwa saa 24, na kutokana na uhaba huo, utaratibu wa vituo vya afya ni kufunguliwa mapema asubuhi na kufungwa saa 9:30 mchana, tofauti na hospitali.

  “Katika hali kama hii inakuwa vigumu kuwashawishi wafanyakazi wetu kuhamia kwenye nyumba hizo, na pia tunakabiliwa na ukosefu wa fedha za kununua samani kwani zile zinazopatikana katika bajeti zinatumika zaidi katika ununuzi wa vifaa vya hospitali,” alifafanua.

  Kwa hivyo alisema, wizara imekuwa ikitafuta wafadhili wengine kuomba msaada wa kuweka vifaa katika nyumba hizo, ambapo hivi karibuni wamefanikiwa kupata samani kwa kituo cha afya Bumbwini Makoba Wilaya ya Kaskazini ‘B’.

  Aidha alisema, kimsingi nyumba hizo zimekusudiwa zikaliwe na wafanyakazi wa kitengo cha huduma za mama waja wazito na uzazi ambazo zinahitaji uangalizi wa saa 24.

  Kwa sasa, alisema ukosefu wa vifaa vya huduma hizo pamoja na samani za nyumba, unakwamisha mpango wa watendaji kuhamia katika nyumba hizo.

  Alitoa wito kwa wahisani wa ndani na nje, wakiwemo pia viongozi wa majimbo husika, kujitokeza kutoa misaada kwa ajili ya vituo vya afya na nyumba za wafanyakazi, ili kuwaondoshea usumbufu wananchi.

  Alisema azma ya serikali ni kuendelea kuwapatia wananchi wake huduma bora za afya kadiri hali ya kifedha inavyoruhusu, kwani inawategemea katika shughuli za kuleta maendeleo.

  IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO

  5 SEPTEMBA, 2016 .
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: AGIZO LA DC ZANZIBAR LAGONGA UKUTA,MADAKTARI WAKWAMA KUHAMIA KIJIJINI Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top