NA Beatrice Lyimo-MAELEZO
Dar es Salaam
WAZIRI
wa Mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Nchemba anatarajia kuwa mgeni rasmi katika
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 47 wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya utakaofanyika
kuanzia Septemba 30 hadi Octoba 2 mwaka huu.
Akizungumza kwa niaba
ya Mkuu wa Jumuiya hiyo Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry, Katibu Mkuu Msaidizi Abdurahman
Ame alisema kuwa mkutano huo utafanyika eneo la kitonga, kata ya Msongola
Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Alisema Jumuiya
imeandaa mkutano huo kwa lengo la kuhamasisha amani katika jamii na
kuwakumbusha waumini hasa wa kiislamu juu ya misingi sahihi ya dini ya kiislamu
pamoja na kumjua na kutimiza haki ya Mwenyezi Mungu.
“Wajibu wa kiongozi
wa dini ni kuandaa na kuhamasisha masuala ya dini, hivyo lengo la mkutano huo
ni kuhamasisha amani katika jamii na pia kuwakumbusha waumini wa kiislamu juu
ya kumjua, kuishi na kutimiza haki ya Mwenyezi Mungu hali itakayosaidia
kuondokana na vitendo viovu,” alifafanua Katibu huyo.
Mbali na hayo,
mkutano huo utabebwa na kaulimbiu isemayo “kuitambua amani ya jirani yako,
huvunjilia mbali kuta zinazowatenganisha” ikiwa na ujumbe ya kwamba kuna haja
ya kuelimisha jamii uzuri wa mafundisho ya dini kwa kutumia vitabu vitakatifu
kupitia vyombo mbalimbali vya masasiliano.
Vile vile, Washiriki mbalimbali
kutoka ndani na nje ya nchi zikiwemo Kenya, Uganda, Burundi, Malawi, Msumbiji
na Uingereza wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za kidini na za
kijamii watashiriki katika mkutano huo.
Ahmadiyya ni jumuiya
ya waislamu ya kimataifa iliyoenea katika nchi 209 duniani kwa lengo la kuleta
uhuisho wa dini ya kiislamu kwa kutangaza kwa amani ujumbe sahihi wa Islam
duniani kote.
0 comments:
Post a Comment