728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Wednesday, September 21, 2016

  Wanafunzi wa Ihungo na Nyakato wapewa uhakika wa kuendelea na masomo.

  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhe. George Simbachawene akiongea na waandishi wa habari (Hawapo pichani) ambapo alisema serikali imewahamisha kwa muda wanafunzi wa shule za Sekondari Nyakato na Ihungo zilizoathiriwa na tetemeko ili kupisha ujenzi upya wa miundombinu katika shule hizo
  Baadhi ya Viongozi wa Serikali na Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhe. George Simbachawene wakati akieleza mikakati ya serikali katika kukarabati miundombinu katika shule zilizoharibiwa na tetemeko lililotokea mkoani Kagera. PICHA NA HASSAN SILAYO-MAELEZO


  Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba.

  Serikali imewahamisha kwa muda wanafunzi wa shule za sekondari Ihungo na Nyakato za mkoani Kagera zilizoharibiwa na tetemeko la ardhi ili kupisha ujenzi upya wa miundombinu ya msingi ya shule hizo.

  Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo Bukoba mkoani Kagera.

  “Shule hizi mbili za Ihungo na Nyakato zimeharibika sana, majengo yote yameharibika hayafai tena kutumika, zinahitaji kujengwa upya na shughuli za ujenzi zimeanza, kazi hiyo inafaywa na vikosi vya JWTZ, Magereza na VETA wameanza kazi katika shule hizo mbili” alisema Simbachawene.

  Waziri Simbaachawene ametaja hatua ambazo Serikali imechukuwa hadi sasa kuwa ni pamoja na kusitisha masomo katika shule hizo mbili, kuwahamisha kwa muda wanafunzi wote 1332 kwenda katika shule 7 tofauti na kuzijenga upya shule hizo ambapo hatua za awali za ujenzi tayari zimeshaanza.

  Waziri Simbachawene amewataja wanafunzi wa shule hizo ambao wanahamishiwa shule nyingine kuwa ni wa kidato cha tano na cha sita.

  Kutokana na athari za tetemeko hilo jumla ya shule 353 majengo yake yameathirika kwa viwango tofauti ambapo kati ya shule hizo, 110 ni za sekondari na 243 ni za msingi.

  Ili kuhakikisha wanafunzi hao wanapata elimu kulingana na ratiba za shule na miataala ya vidato vyao, jumla ya idadi ya wanafunzi 748 kutoka shule ya sekondari Ihungo, kati yao wanafunzi 372 ni wa kidato cha sita na 376 ni wa kidato cha tano.

  Waziri Simbachawene ameongeza kuwa kati ya wanafunzi hao wa Ihungo 649 ni wa Tahasusi za masomo ya sayansi na 99 masomo ya sanaa ambapo walimu wanaofundisha shule hiyo idadi yao ni 31.

  Kwa upande wa shule ya Sekondari Nyakato, Waziri Simbachawene amesema kuwa wapo jumla ya wanafunzi 567 wakiwemo wanafunzi wa 388 wa masomo ya sayansi na 179 masomo ya sanaa ambapo idadi hiyo inajumuisha wanafunzi 227 wa kidato cha sita na 340 wa kidato cha tano na kuna jumla ya walimu 32.

  Ili kutoathiri mwenendo na hatua za wanafunzi kujifunza, Waziri Simbachawene amesema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI imewasambaza wanafunzi hao kwenda shule za sekondari Kahororo na Omumwini zote za Manispaa ya Bukoba, Biharamulo na Nyakahura kutoka halmashauri ya Biharamulo, Kishoju na Nyailigamba halmashauri ya Muleba na Chuo cha Ualimu cha KKKT Bukoba.

  Kufuatia hatua hiyo ya kuwahamisha wanafunzi hao, Waziri Simbachawene amesema kuwa wanapaswa kuripoti katika shule hizo Oktoba 1, 2016 badala ya Septemba 26 ya awali ili kuruhusu madogomadogo ya miundombinu katika shule hizo.

  Wanafunzi hao watasoma katika shule hizo hadi mwezi Desemba 2016 hatua ambayo inatarajiwa ujenzi wa miundombinu ya msingi itakuwa imekamilika na kuruhusu wanafunzi kurejea kwenye shule zao Januari 2017 ambapo shule zote nchini zitafunguliwa kwa pamoja.

  Aidha, Waziri Simbachawene amewataka walimu, wanafunzi na wanajamii katika shule walizopokea wanafunzi hao, wawe faraja kwa watoto hao washirikiane nao na kuishi kindugu.

  Orodha ya majina ya wanafunzi waliohamishwa shule watatolewa kwa njia ya vyombo vya habari pamoja na kuwekwa kwenye tovuvi ya Ofisi ya Rais TAMISEMI www.tamisemi.go.tz na wanapaswa kuendelea kutumia sare zao za awali.

  Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Juma Kaponda amesema kuwa walimu wa shule za Ihungo na Nyakato wataambatana na wanafunzi wao walipopangiwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Wanafunzi wa Ihungo na Nyakato wapewa uhakika wa kuendelea na masomo. Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top