728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Tuesday, September 27, 2016

  WADAU WA HABARI WAIPONGEZA SERIKALI.

  Na Abushehe Nondo, MAELEZO.

  Wadau wa habari nchini wameipongeza Serikali kwa kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Huduma za habari wa mwaka 2016.

  Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) Bw. Theophil Makunga wakati akitoa taarifa kuhusu muswada wa Sheria ya huduma za habari wa mwaka 2016 kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.

  “Tunaishukuru Serikali kwa kuanza mchakato wa kuiondoa sheria ya habari ya mwaka 1976 kwa kupeleka bungeni muswada mpya wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016” Alisema Makunga.

  Alisema kuwa muswada huo ambao umesomwa bungeni kwa mara ya kwanza na Waziri wa habari ,Utamaduni , Sanaa na Michezo Nape Nnauye utamaliza kilio cha siku nyingi cha waandishi na wadau wa habari kuhusu sheria ya mwaka 1976 ambayo ilionekana kuwabana katika utendaji wao wa kazi.

  Ameongeza kuwa katika muktadha huo, taasisi mbalimbali za kihabari na wadau wa habari wanatakiwa kushiriki katika kutoa maoni yao ili kazi ya uandishi wa habari isiwe na matatizo.

  Makunga amesisitiza kuwa muswada huo siyo mali ya wamiliki wa vyombo vya habari , wahariri, au vyumba vya habari vilivyopo Dar es Salaam pekee bali unagusa maslahi mapana ya sekta nzima ya habari nchini.

  Aidha, katika kukusanya maoni hayo ya wadau wa habari wamewekewa mpango utakaowawezesha kukusanya maoni yao nchi nzima kupitia klabu zao za waandishi wa habari zilizosambaa nchi nzima.

  Wadau wa habari nchini wataweza kusoma muswada huo na kufanya uchambuzi wa maudhui yake na hatimaye kutoa maoni yatakayowezesha kupatikana kwa sheria bora.

  Muswada wa Sheria ya huduma za habari wa mwaka 2016 kwa mara ya kwanza umesomwa bungeni na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye katika Mkutano wa Nne wa Bunge la 11 lililomalizika Septemba 16 mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: WADAU WA HABARI WAIPONGEZA SERIKALI. Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top