728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Monday, September 19, 2016

  UWANJA WA TAIFA WAONGOZA KWA UBORA ZAIDI KATIKA KANDA YA AFRIKA MASHARIKI.


  Na Anitha Jonas – WHUSM

  Heko Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo kwa kusimamia ujenzi wa mageti ya kielektroniki katika kuboresha makusanyo yatokanayo na michezo iinayofanyika Uwanja wa Taifa.

  Hizo ni pongezi zilizokuwa zikitolewa kwa uongozi wa Wizara kutoka kwa wadau wa michezo hivi karibuni mara baada ya kuzinduliwa kwa mfumo wa kisasa wa mageti ya kieletroniki ambayo hutumia kadi maalumu ambazo ndiyo huruhusu mageti kufunguka na mtu kupita.Hivyo basi namna hiyo ya mageti hayo yanavyofanya kazi ndiyo huleta tafsiri ya mfumo wa mageti ya kieletroniki.

  Akizungumza katika makabidhiano ya mageti hayo ya kieletroniki yaliyoko katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Mhe.Nape Moses Nnauye alisema kwa kufanikisha hilo kumeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuwa na mageti ya kisasa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki. Na hii ni sehemu nzuri.

  Kukamilika kwa ujenzi wa mageti hayo kunafuatiwa na agizo la Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kikazi uwanjani hapo mnamo Februari 17,2016 na kumwagiza Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakamilika kwa haraka kwa kuwa ni sehemu ya mkataba wa ujenzi wa uwanja.

  Pamoja na hayo Waziri Nnauye alieleza kuwa mfumo huo umeandaliwa na Kampuni ya kizalendo ya SELCOM Tanzania ambapo hao ndiyo watakao kuwa wasambazaji wa Kadi hizo kwa nchi nzima na kadi hizo zitakuwa zikipatikana kwa mawakala wao wote na zitatolewa bure pasipo kugharamia kiasi chochote cha fedha bali kitakacho hitajika ni kuzijaza kadi hizo fedha.

  “Kwa niaba ya Waziri Mkuu napenda kuwasilisha pongezi zake kubwa kwa Kampuni ya China ya BCEG kwa kukamilisha mradi huu wa mageti ya kisasa kama ilivyokuwa sehemu ya ujenzi wa uwanja mbali na kupitia changamoto mbalimbali,pongezi nyingi pia kwa Kampuni ya SELCOM kuifanya kazi hii kwa uaminifu mkubwa,”alisema Waziri Nape.

  Kwa upande wa namna ya matumizi ya kadi hizo mdau yeyote wa mpira atahitajika kusajili kadi yake kwa kutoa taarifa zake binafsi za muhimu ikiwa ni pamoja na namba yake simu ambapo taarifa hizo zitahifadhiwa na na itakapotokea kadi yako imechukuliwa na mtu mwingine yoyote na kufanya malipo yoyote ujumbe utaingia kwenye simu yako kukutaarifu kuwa kadi yako inafanya malipo na hii ni kwa sababu kadi hizi zina uwezo wa kutumika kwa vitu mbalimbali ikiwemo kulipa bili za maji,kununua LUKU,kununulia mafuta katika vituo mbalimbali pamoja na kununulia vocha.

  Pia mara baada ya kufika uwanjani hapo kitakachohitajika kwa mtu yeyote atakayefika uwanjani kwa lengo la kuingia kushuhudia mechi ni kuweka kadi yake kadi kifaa maalum kilichopo katika mageti hayo ambacho ndicho kinachofungua na kufunga mageti hayo.

  Pamoja na hayo ilielezwa kuwa kila mdau wa michezo inayofanyika uwanjani hapo atakuwa na uwezo wa kukata tiketi kupitia kadi yake kulingana na uwezo wake na atachagua ni sehemu gani ya viti atakapoketi kulingana na tiketi aliyokata kama ni VIP au viti vya Bluu au Rangi ya Chungwa (Orange) kutakuwepo na mashine maalum za kutambua ni wapi utaketi kulingana na tiketi yako.

  Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Prof.Elisante Ole Gabriel aliwatoa hofu watanzania katika sherehe za makabidhiano ya mageti hayo kwa kusema kadi hizo zitaweza kumilikiwa na kila mtu na siyo kwa watu maalum tu kwani kadi hiyo ndiyo itakayompa mtu yeyote uwezo wa kuingia uwanjani hapo.

  Mfumo huu utakuwa na faida zifuatazo mbali mbali kama Kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya mechi zinazofanyika uwanjani hapo tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kulikuwepo na wizi wa tiketi ambao ulichangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha zoezi la ukusanyaji wa mapato kwani kwa sasa pale mtu anapokata tiketi tu pesa hiyo inaigia moja kwa moja na kufanyiwa mgao kupitia mtandao bila kujali mtu huyo atahudhuria mechi hiyo au la.

  Faida nyingine ni kuimarisha usalama zaidi kwani awali pesa zilizokuwa zikikusanywa kwa makato ya tiketi zilikuwa zikihitaji ulinzi mkubwa katika kuzihesabu na kuzihifadhi na kuzigawa kwa wadau wanaonufaika na mgao wa mapato yatokanayo na mechi, pamoja na taarifa za watu watu wote watakaoingia uwanjani zitakuwa zimehifadhiwa katika mfumo.


  Vile vile matumizi ya yatarahisisha kupunguza foleni na kuweza kupitisha watu wengi zaidi kwa muda mfupi tofauti na ilivyokuwa awali. Hivyo itapunguza kero kwa mashabiki wanaofika uwanjani hapo kutizama mechi kukaa muda mrefu katika mistari ya kuingia uwanjani.Hakika kutumika kwa mfumo huu kutasaidia kuendeleza huduma za michezo nchini na kufikia kiwango cha Kimataifa .

  Katika mazungumzo ya moja kwa moja na Meneja Mradi wa Ujenzi wa Mageti hayo kutoka SELCOM Bw.Gallus Runyeta alitoa wito kwa watanzania kufika kwa mawakala wao kwa ajili ya kujipatia kadi hizo mapema kabla ya kufufikia siku za mechi ili kuondoa usumbufu wowote ambao ungeweza kujitokeza.Pia alieleza kuwa kadi hizo zinatarajiwa kuanza kutumika kwa majaribio katika mechi ya Simba na Yanga itakayofanyika uwanjani hapo Oktoba Mosi mwaka huu.

  Naye Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchi Bw.Jamal Malinzi aliipongeza serikali kwa kuanzisha mfumo huo wa kisasa wa kukusanya mapato kwani utasaidia kupunguza kelele za mgao tofauti na awali na pia aliiomba serikali kuhakikisha mgao huo unawafikia wadau husika kwa wakati kwani vilabu huhitaji pesa hizo kwa haraka sababu ndiyo wanazozitegemiea katika uendeshaji wa shughuli zao.

  Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya BCEG nchini Bw. Cheng Long Hai ambayo ndiyo kampuni iliyojenga uwanja huo aliishukuru serikali kwa kuipa ushirikiano katika kipindi cha ujenzi wa uwanja huo na kuahidi kusimamia vyema matumizi ya mageti hayo kwa kipindi cha mwaka kama walivyotiliana saini katika mkataba na serikali.

  Pia alisema kuwa anajivunia kwa kiasi kukubwa kujenga uwanja huo ambao ameweza kukamilisha kama mkataba ulivyokuwa unasema na hii ni faraja kwake kuweza kutimiza kila ilichohitajika kulingana na uhitaji na aliendelea kusema kuwa kuwepo kwa mageti hayo ya kisasa katika uwanja huo kunaufanya uzidi kuoneka wa kisasa zaidi barani Afrika na kwa Kanda ya Afrika Mashariki.

  Naye mmoja wa wadau wa soka nchini Bw. Hussein Makame mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam alitoa maoni yake kwa kuuomba uongozi wa SELCOM kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kutumia kadi hizo kabla ya siku za mechi kwa uwezo wa uelewa wa kila mtuaingiea uwanjani pale ni tofauti na kwa kufanya hivyo watapunguza usumbufu.


  Pamoja na hayo, Bw. Hassan Silayo, mkazi wa Kimara Suka jijini Dar es Salaam ambaye nae ni mkereketwa wa soka la nchini aliishauri serikali kuweka ulinzi wa kutosha katika mageti hayo kwa siku ya kwanza kutakapokuwa na mechi kwa lengo la kulinda waharibifu wa miundombinu hiyo; kwani kumekuwa na kawaida ya baadhi ya mashabiki wanapofungwa kuharibu miundombinu pia alitoa pongezi nyingi kwa serikali kwa kuleta maendeleo kama hayo katika sekta ya michezo.

  Hata hivyo mpaka sasa SELCOM wameshatoa kadi za viongozi wakuu nchini za kuingilia katika mageti ya uwanja huo akiwemo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu ambapo kadi zao alikabidhiwa Waziri wa Habari wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.Nape Moses Nnauye kwa ajili ya kuwapatia viongozi hao katika sherehe za makabidhiano ya mageti hayo kwa serikali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: UWANJA WA TAIFA WAONGOZA KWA UBORA ZAIDI KATIKA KANDA YA AFRIKA MASHARIKI. Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top