728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Tuesday, September 20, 2016

  UVCCM YAWAVUA KATIBU NA MWENYEKITI ARUSHA

  KAMATI ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa, limependekeza kwa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) kumvua uongozi Mwenyekiti wa umoja huo mkoani Arusha, Lengai Ole Sabaya, kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kufikishwa mahakamani akituhumiwa kwa utapeli. 

  “Wakati tukisubiria uamuzi wa Chama, Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa imemsimamisha uongozi wa nafasi yake ndani ya UVCCM kutokana na kesi iliyoko Mahakamani na kumtaka kuanzia leo (jana) asijihusishe na shughuli zozote za uongozi wa UVCCM hadi hatima ya tuhuma zake itakapoamuliwa na Mahakama na vikao husika vya UVCCM na CCM. 

  Mbali na Sabaya, UVCCM pia imemtimua kazi aliyekuwa katibu wake mkoani humo kwa kukiuka utaratibu na maagizo ya UVCCM na CCM ikiwemo vitendo vya utovu wa nidhamu. 

  Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana Dar es Salaam na kutiwa saini na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, ilisema Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa ilikutana Septemba 19, nwaka huu Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Sadifa Juma Khamis ambapo pamoja na mambo mengine walifikia uamuzi huo. 

  Ilisema kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha Kamati ya Maadili na Nidhamu ya UVCCM Taifa, ambapo pamoja na mambo mengine kilipokea na kujadili uhai wa CCM na umoja huo mkoani Arusha. Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo walijadili kuyatolea ufafanuzi mambo mbalimbali kuhusu makada wake hao wawili. 

  Taarifa ya Shaka ilisema miongoni mwa mambo yaliyomhusu Sabaya ikiwemo kuyaongoza makundi ya vijana wa CCM na wasiokuwa wa CCM ili kumkataa Katibu wa UVCCM aliyehamishiwa mkoani Arusha, Said Goha kuchukua nafasi ya Ezekiel Mollel. Ilisema kuwa Sabaya licha ya kupewa heshima na kuelimishwa na vikao vya juu na viongozi mara kwa mara kupitia Mwenyekiti wa UVCCM taifa, kuhusu mamlaka za kikanuni ikiwemo ya utumishi na maadili ya UVCCM lakini ameshindwa kujirekebisha. 

  “Sabaya amesababisha taharuki iliyosababisha ofisi za UVCCM Arusha kufungwa kwa minyororo hadi Jeshi la Polisi kuingilia kati. Vile vile taharuki hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa Vijana wa mkoa wa Arusha kugawanyika katika makundi na kusababisha hali ya usalama na maadili kwa umoja huo na Chama kuwa ya wasiwasi. 

  “Sabaya kufikishwa mahakamani akikabiliwa na mashitaka mawili likiwemo la kujifanya mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa. Huku kosa la pili katika muda usiojulikana akidaiwa kughushi vitambulisho vya Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) chenye namba MT 86117 wakati akijua ni kinyume cha Sheria za nchi. 

  “Kamati ya Utekelezaji ilipitia tuhuma mbalimbali na vielelezo vya utapeli na ulaghai unaodaiwa kutendwa na Sabaya katika maeneo tofauti huku akijua ni kinyume na miiko na maadili ya uongozi wa UVCCM na CCM.
  “Kwa makosa yote hayo Sabaya amekukiuka kanuni ya uongozi na maadili ya CCM Fungu la (3) ukurasa wa 16 na 17, na fungu la (4) ukurasa wa 29, 30 na 31. Pia makosa hayo ameyatenda kinyume na utaratibu wa uongozi na maadili ya UVCCM, Ibara ya 6.3.2 Ibara ya 7.5.1, 7.5.4 na 8.2.5,”alisema.


  Kuhusu Mollel, alisema alipokuwa Katibu wa Vijana Mkoa wa Arusha, alipewa barua ya uhamisho, kama inavyoelekezwa na Kanuni ya Utumishi ya UVCCM kifungu cha 3(13) ukurasa wa 21 na 22 inayohusu uhamisho wa mtumishi. Kanuni hiyo inasema “Mfanyakazi yeyote atakayekataa kutii amri ya uhamisho bila sababu zinazokubalika atachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni hizi”. Ilisema Mollel amerudia makosa mara kwama kwa kuwa aliwahi kusimamishwa kazi mwaka 2015 akiwa Katibu wa UVCCM Mkoa wa Manyara, jambo ambalo lilisababisha kumnyang’anya kituo na kumsimamisha kazi kwa muda. 

  Aidha, pamoja na yote hayo Mollel hakujirekebisha hata pale aliporudishwa kazini na kupelekwa mkoa wa Arusha. “Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Taifa imebariki uamuzi uliochukuliwa na Sekretarieti ya Baraza Kuu ya UVCCM iliyokutana Septemba 14, mwaka huu. Kamati imependekeza kwa Baraza Kuu la UVCCM Taifa kumfukuza kazi mara moja Ezekiel Mollel,”ilisema.

  Aidha ilitoa ufafanuzi kuuhusu madai ya tuhuma zinazotolewa na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha kuwa kuna ufisadi na baadhi ya viongozi wa makao makuu ya UVCCM wanahusika ilisema ikumbukwe kuwa umoja huo ulianza kujitathimini na kuhakiki mali zake Desemba, 2015.

  Ilisema mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa iliyobainika kuwa taarifa zake hazikuwa na ukweli na kubainisha matakwa ya uhakiki kama walivyoagizwa.

  Kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa kilichokutana tarehe 18/08/2016 Mjini Dodoma kupokea na kupitia taarifa za uhakiki Mali za UVCCM ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya kiliagiza Sekretarieti ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa kuwaita Viongozi wa Mkoa wa Arusha ili kuendelea kujiridhisha na taarifa walizowasilisha Makao Makuu kwa vile zimebainika kuwa na mapungufu makubwa.

  Katika Taarifa hiyo iliyowasilishwa kwa maandishi na kuthibitishwa na Kamati ya Utekelezaji ya Mkoa wa Arusha hakuna sehemu ambayo kumeainishwa ubadhirifu ama upotevu wa fedha kinyume na madai yaliyoibuliwa siku za karibuni baada ya Viongozi hao kuchukuliwa hatua za kinidhamu, kutokana na makosa ya Maadili ya Uongozi.

  Hata Kamati ya Utekelezaji ya Mkoa wa Arusha ilipoitwa katika kikao cha Kamati ya Maadili cha tarehe 19/08/2016 kilichofanyika Mjini Dodoma walikana na kudai wao hawajawasilisha malalamiko yoyote kuhusu tuhuma wanazozitoa na kusema wanaendelea na kufanyia kazi na kurekebisha mambo ya msingi kuhusu Uchumi wa Mkoa wao.

  Kufuatia hatua hiyo Kamati ya Maadili na Nidhamu na Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa iliagiza Ofisi ya Katibu Mkuu iendelee kufuatilia kwa karibu jambo hilo ili kubaini ukweli baada ya kujiridhisha kuweko na harufu ya ubadhirifu, jambo ambalo limepelekea Viongozi hao kutosema ukweli pamoja na kusisitizwa mara kadhaa kwa maandishi bado taarifa zao hazikujitosheleza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: UVCCM YAWAVUA KATIBU NA MWENYEKITI ARUSHA Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top