728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Thursday, September 15, 2016

  Tanzania imeweza kupunguza zaidi ya tani 216 za kiasi cha matumizi ya kemikali haribifu

  Na Beatrice Lyimo, MAELEZO, Dodoma.
   
   
  Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba amesema kuwa Tanzania imeweza kupunguza zaidi ya tani 216 sawa na asilimia 86 ya kiasi cha matumizi ya kemikali haribifu chini ya programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya kemikali hizo.

  Waziri Makamba ameyasema hayo leo mjini Dodoma kuelekea kilele cha   maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni Septemba 16, mwaka huu.
  Waziri Makamba amesema kuwa upungufu huo umetokana na jitihada za utekelezaji wa mpango wa usimamizi wa vipozi uliowezesha uwekaji wa mtambo wa kunasa na kurejeleza kemikali uliopo katika kituo cha Tanzania cha uzalishaji bora na teknolojia endelevu.

  Aidha, Waziri Makamba alisema kuwa mpango huo uliwezesha ununuzi na usambazaji wa mashine 20 za kunasa na 5 za kunasa na kurejeleza gesi katika karakana 20 na vituo vitano vya kanda vya kunasa na kusafisha gesi chakavu za majokofu na viyoyozi katika vyuo vya VETA vya Mwanza, Dar es Salaam, Kigoma, Mbeya na Mkokotoni Zanzibar.

  Mbali na hayo, Waziri Makamba ametoa wito kwa wananchi kushiriki katika kupunguza na kuondosha madhara ya Tabaka la Ozoni yanayosababishwa na bidhaa zinazotumika majumbani au sehemu za biashara.

  Waiziri Makamba amesema kuwa ili kuhifadhi tabaka la Ozoni nchini, jamii kwa ujumla inapaswa kuepuka kuingiza gesi zilizopigwa marufuku nchini sambamba na vifaa vinavyotumia gesi haribifu ikiwemo majokofu na viyoyozi vilivyokwishatumika na ambavyo vinatumia vipoozi aina ya R11 NA R12.

  Aidha, wananchi wametakiwa kuepika kutupa ovyo majokofu ya zamani ama vifaa vya kuzima moto vyenye kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni aina ya CFCs na halon na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mafundi ama mamlaka husika.

  Kila mwaka, Septemba 16 Tanzania inaungana na Jumuiya ya kimataifa huadhimisha siku ya Kimataifa ya Hifadhi la Tabaka la Ozoni kama ilivyoagizwa na Mkutano Mkuu wa Ummoja wa Mataifa katika Azimio nambari 49/114 la 19 Desemba 1998 ikiwa kumbukumbu ya kutiwa saini Mkataba wa Montrel kuhusu kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Hewa ya Ozoni angani
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Tanzania imeweza kupunguza zaidi ya tani 216 za kiasi cha matumizi ya kemikali haribifu Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top