JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


SERIKALI ILIVYOJIDHATITI KATIKA UJENZI WA MAGHALA YA VYAKULA NCHINI

Share This
Na Ismail Ngayonga- MAELEZO.
SEKTA  ya kilimo inayojumuisha ukulima, ufugaji na uvuvi, imeendelea kuwa sekta kiongozi katika kutoa ajira na kuwa tegemeo la maisha kwa asilimia 75 ya Watanzania wanaoishi Vijijini.

Kujitosheleza kwa chakula ni muhimu kwa usalama na utulivu wa nchi. Taarifa ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi zinaonyesha kuwa kiwango cha kujitegemea kwa chakula kimeongezeka kutoka asilimia 95 mwaka 2005 hadi asilimia 125 mwaka 2014. 

Pamoja na uzalishaji kuwa mkubwa, inaelezwa kuwa kiasi kikubwa cha mazao ya nafaka yanayozalishwa nchini  huharibika na kupotea baada ya kuvunwa. Upotevu huo hutokana na matumizi ya mbinu duni za kuhudumia mazao wakati wa uvunaji, usafirishaji na uhifadhi kwenye maghala.

Uzalishaji wa mazao ya nafaka unakadiriwa kufikia wastani wa tani 3, 897,500 kwa mwaka na asilimia 80 ya nafaka huzalishwa na kuhifadhiwa vijijini, ambapo hata hivyo uwezo mdogo na maghala duni yanayotumiwa na wakulima vijijini wakati wa kuhifadhi huruhusu upotevu wa nafaka hadi asilimia 10.

Takwimu za Shirika la Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) zinaonyesha kuwa, asilimia 30 hadi 40 za nafaka zinazovunwa hupotea kila mwaka nchini.

Mahindi ni miongoni mwa  mazao makuu ya nafaka hapa nchini yanayolimwa nchini Huzalishwa kwa wastani wa tani 2,393,000 kwa mwaka ambao ni sawa na asilimia 63 ya mazao yote ya nafaka.

Takwimu za Wizara ya Kilimio, Mifugo na Uvuvi zinaonyesha uzalishaji wa mahindi unaongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, mwaka 2011 uzalishaji wa mahindi katika nchi nzima ulifikia tani 4,341, mwaka 2012 tani 5,104 na mwaka 2013 tani 5,174.

Taarifa kutoka mikoa ya Rukwa na Katavi zinaeleza kuna uwezekano mkubwa wa kuharibika kwa tani 40,000 za mahindi yanayoendelea kununuliwa katika msimu huu na Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kutokana na uhaba wa maghala ya kuhifadhi.

Wakala katika mikoa hiyo anakabiliwa na changamoto ya uwezo mdogo wa kuhifadhi chakula hicho katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mahindi na kusababisha akiba kubwa ya chakula kuhifadhiwa nje ya maghala.

Utafiti uliofanywa na mradi wa USAID Tuboreshe Chakula umebaini kuwa kutokana na uhifadhi duni na mbinu bora za kilimo cha mazao ya nafaka kama mahindi, alizeti na maharage unasababisha ukungu kwenye mazao hayo  hali inayosababisha sumu kuvu yenye madhara makubwa kwa mlaji.

Mhadhiri Mwandamizi wa chuo kikuu cha sayansi cha Nelson Mandela, Dk. Martin Kimanya anasema sumu hiyo haiwezi kuondolewa kwa kupika chakula na badala yake watumiaji wanapaswa kuchagua nafaka kwa kuondoa zile ambazo zimebadilika rangi na kuwa na ukungu.

“Wakati Tanzania ikiwa katika nafasi ya nne kwa ulizalishaji wa zao la mahindi barani Afrika, imeelezwa kuwa watumiaji wa mahindi wanakula 30% ya sumu kuvu inayotokana na uhifadhi duni wa mahindi” anasema Prof Kimanya.

Kutokana na tatizo hilo mradi wa USAID tuboreshe chakula umeanza mikakati ya kuinusuru jamii ikiwemo kwa kutoa elimu kwa wasindikaji wa vyakula pamoja na wakulima ili kufahamu sumu kuvu na madhara yake.

Katika  kuongeza na kuimarisha uhakika na usalama wa chakula nchini, Serikali kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula Nchini (NFRA) imepanga kujenga maghala 275 kwa awamu katika sehemu zenye uzalishaji mkubwa wa zao la mahindi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anasema Serikali imejipanga katika kuondoa tatizo la upungufu wa chakula nchini kwa kujenga magala mengi zaidi ya kuhifadhi chakula katika maeneo mbalimbali yenye changamoto za upungufu wa chakula.

“Serikali  kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea kujenga maghala ya kimkakati kwa ajili ya kuhifadhi akiba ya Taifa na kwa sasa ghala moja lenye uwezo wa kuhifadhi Tani 5,000 limeshajengwa Wilayani Mbozi Mkoani Mbeya ” anasema Majaliwa

Aidha Majaliwa anasema Serikali imepata mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland ambao utawezesha kujenga vihenge vya kisasa (silos) vyenye uwezo wa kuhifadhi Tani 160,000 na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi Tani 90.

Anasema maghala yanakayojengwa si kwa ajili ya kuhifadhi chakula tu bali hata kuweka dawa kwa urahisi, kukausha, kuondoa unyevunyevu na kusafisha kwa kiwango kinachohitajika.

Waziri Mkuu anasema kuwa anasema ujenzi wa magahala hayo utaliongezea taifa uwezo wa kuhifadhi chakula tofauti na hali ilivyo sasa.

Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba  anasema Serikali imeiagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA)  kununua mahindi moja kwa moja kutoka  kwa wakulima na kuachana na mfumo wa zamani ambapo wakulima walikuwa wakipeleka mahindi kwenye wakala huo au kupitia kwa wanunuzi binafsi.

Kwa mujibu wa Waziri Tizeba anasema mkulima atauza kuanzia tani moja hadi mbili na kiwango cha mwisho cha ununuzi kufanywa na NFRA  ni tani tano.

Aidha Dkt. Tizeba anasema  serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni kumi kwa ajili ya ununuzi wa mahindi kutoka kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini. 

Mary Sheto kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi anasema Serikali imeweka mikakati madhubuti kwa ajili ya kuwasaidia wananchi maskini waliopo  vijijini ambao asilimia 98 hutegemea kilimo kama njia kuu ya uchumi na maisha yao ya kila siku. 

Anasema lengo la Serikali ni kuzalisha tani milioni tano za mahindi ili nchi ijitosheleze kwa chakula kwa nia ya kupunguza mfumuko wa bei ya chakula na kuongeza kipato kwa mkulima hatimaye kukuza uchumi  na kuuza ziada ndani na nje ya nchi ambako imebainika kuwa na soko kubwa la mazao hayo.

Kwa mujibu wa Sheto anasema Serikali imefanya mazungumzo na Shirika la Chakula Duniani (WFP) kwa ajili ya ununuzi wa mahindi hayo na wameonesha kukubali, lakini kwa masharti ya kuzingatia ubora wa mahindi husika.

“Kwa kuzingatia hilo, Serikali katika wilaya ambazo zitaanzishiwa utaratibu huo, wakulima wataelekezwa namna ya kuandaa zao hilo kwa ubora unaotakiwa kisha kuwahimiza kuwa katika vikundi huko huko vijijini ambako ununuzi utafanyika” anasema Sheto.

Akifafanua zaidi Sheto anasema Serikali itahakikisha maghala mapya yanajengwa na yale ya zamani yataboreshwa kwa kukarabatiwa, ili mahindi yawe katika mazingira safi kwa lengo la kumvutia mnunuzi atakayenunua zao hilo katika soko la pamoja la wakulima.

Anaitaja Mikoa itakayofaidika na mpango huo kuwa ni Rukwa /Katavi, Ruvuma, Njombe na Iringa, mikoa ya Kanda ya Ziwa, Dodoma na lingine katika mikoa ya Tanga/Arusha na Kilimanjaro.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad