728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Monday, September 19, 2016

  Mradi wa YEE waisaidia Temeke kupunguza wahalifu

   Afisa Maendeleo ya Jamii – Kata ya Vingunguti, wilayani Temeke Pius Majura akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu maendeleo ya vijana waliohitimu mafunzo ya ufundi katika Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA) chini ya mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE).
  Afisa Mtendaji wa Kata ya Sandali iliyopo wilayani Temeke, Engerasia Lyimo akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) ulivyowanufaisha vijana katika kata hiyo.    Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

  Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) unaofadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) umeisaidia Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kupunguza idadi ya wahalifu kwa kuwapatia vijana elimu ya mafunzo ya ufundi inayowawezesha kuendesha maisha yao.

  Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Afisa Maendeleo ya Jamii – Kata ya Vingunguti, Pius Majura alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya vijana waliohitimu mafunzo ya ufundi katika Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA) chini ya mradi huo.

  Majura amesema kuwa mradi huo umewasaidia vijana wa eneo hilo kuacha kufanya uhalifu na badala yake wamejikita katika shughuli za halali ambazo zinawasaidia kupata kipato cha kuwawezesha kuendesha maisha yao.

  “Kabla ya mradi huu kuanza vijana wengi walikuwa wakijihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya na wasichana wengi walikua wakifanya biashara za kuuza miili yao, madanguro yalikuwa mengi lakini baada ya vijana kupatiwa elimu na wengine kuweza kujiajiri na kuajiriwa, uhalifu umepungua kwa asilimia kubwa”, alisema Majura.

  Afisa huyo ameongeza kuwa Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kupunguza utegemezi kwa kuwasaidia vijana na wanawake kuweza kusimama wenyewe kwa kufanya shughuli zao mbalimbali hivyo, wametenga fungu la fedha kwa ajili ya makundi hayo ili kuhakikisha wanajikwamua wao binafsi pamoja na taifa kwa ujumla.

  Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Sandali iliyopo wilayani humo, Engerasia Lyimo amesema kuwa mradi huo umewafanya vijana wajielewe na kujitambua wao ni kina nani pia umepunguza idadi ya watoto wa mitaani waliokuwa wakirandaranda bila kuwa na shughuli maalum hali iliyokuwa ikiwapelekea kujiingiza katika makundi ya uhalifu.

  Ametoa rai kwa Shirika la Plan International kupanua wigo wa maeneo wanayoyasaidia kwani bado kuna kata nyingi za wilaya hiyo hazijapata fursa za kuingizwa katika mradi huo.

  Mradi huo wa miaka mitatu unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Mradi wa YEE waisaidia Temeke kupunguza wahalifu Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top