728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Tuesday, September 27, 2016

  MKUU WA MKOA AZINDUA MIRADI YA MAJI KWA AJILI YA VIJIJI VYA SARANDA NA SUKAMAHELA NA KUPIGA MARUFUKU BIASHARA YA MKAA WILAYANI MANYONI.

  Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe akipampu maji katika kisima cha maji cha Kijiji cha Sukamahela kilichokarabatiwa na taasisi ya peace corps pamoja na wanakijiji wa Sukamahela, usambazaji wa maji kutoka katika kisima kwenda kijijini unafanywa na shirika la Wolrd Vision.

  Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe akipanda mti katika chanzo cha maji cha kijiji cha Saranda ili kutunza mazingira ambapo ukarabati na usambazaji wa maji kutoka katika chanzo hicho kwenda kijiji cha Saranda unafanywa na shirika la Wolrd Vision.  Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe akizungumza na wakazi wa kijiji cha Sukamahela na kuwasisitiza kutunza mazingira na kuachana na biashara ya mkaa kwani huharibu mazingira kwa kukata miti kwa wingi.
  Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe akipokea maelekezo ya kusimamia wananchi wake kutofanya biashara ya Mkaa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe wakati wa kikao na wakazi wa kijiji cha Sukamahela, kushoto kwakwe ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Manyoni na anayefuata ni Meneja wa Wolrd Vision kanda ya kati Faraja Kulanga.

  ……………………………………………………………………..

  Na Grace G. Singida

  Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe amepiga marufuku biashara ya mkaa wilayani Manyoni kutokana na ukataji miti hovyo unaoharibu vyanzo vya maji na kumwelekeza Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe kusimamia utekelezaji wa agizo hilo.

  Mhandisi Mtigumwe ametoa agizo hilo katika vijiji vya Sukamahela na Saranda wilayani Manyoni wakati akizindua miradi miwili ya maji ambapo shirika la wolrd vision litatoa milioni 355 shirika la peace coarps limetoa shilingi milioni sita na wananchi wakichangia milioni mbili.

  Amesema kumekuwa na tabia ya ukataji miti hovyo kwa ajili ya biashara ya mkaa hasa kwa halmashauri hiyo na kuwataka wananchi kuangalia ujasirimali mwingine huku wakiruhusiwa kukata mkaa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani tu.

  Mhandisi Mtigumwe ameongeza kuwa kamati za miradi hiyo ya maji zinapaswa kusimamia moiradi hiyo na kutoa elimu ya uitunzaji wa mazingira kwa jamii inayozunguka miradi hiyo ili iweze kuwa endelevu.

  Amesema kamati hizo zipange bei ya kuuzia maji itakayokuwa rafiki kwa wana jamii wote ili miradi hiyo iwanufaishe wananchi hao na kupata pesa ya kuendeshea jenerator na utunzaji wa miundombinu kwa pesa itakayokusanywa.

  Mhandisi Mtigumwe amemshauri Mkuu wa Wilaya hiyo kusimamia mapato na matumizi ya pesa za miradi hiyo ya maji kutokana na kamati nyingine kufuja pesa za miradi ya maji kasha kuitelekeza bila ya kuiendeleza.

  Meneja wa kanda ya kati wa shirika la World Vision Faraja Kulanga amesema tayari shirika hilo limeshatenga shilingi milioni 150 zitakazo tolewa kuanzia mwezi oktoba kwa ajili ya kutengeneza mifumo na maeneo ya kuchotea maji katika vijiji vya sukamahela na Saranda.

  Kulanga amesema shirika hilo limeshakarabati mradi wa maji wa Saranda ambao tayari unatumika huku shirika likiendelea kukarabati miundombinu ya miradi hiyo na kuzisisitiza kamati za maji kumiliki na kuitunza miradi hiyo kwani wafadhili huondoka.

  Naye mwenyekiti wa kamati ya maji kijiji cha Saranda Julius Kundule amesema kamati hiyo tayari ina shilingi milioni mbili kwenye akaunti huku wakiahidi kuitunza miradi hiyo.

  Kundule ameongeza kuwa kamati hiyo itajitahidi kutunza miradi hiyo na kutoa elimu kwa wananchi juu ya uchangiaji wa maji ili kupata pesa kwa ajili ya ukarabati na utunzaji wa miundombinu kwakuwa wengi hudhani maji ni bure.

  Wakazi wa vijiji vya Sukamahela na Saranda wameyashukuru mashirika ya world vision na peace corps kwa kukarabati miradi hiyo na kusogeza huduma ya maji karibu na makazi yao.

  Wameongeza kuwa uboreshaji wa huduma hiyo ya maji utasaidia kupunguza muda wa kutafuta maji na hivyo kupata muda wa kutosha wa kujishughulisha na miradi ya maendeleo badala ya kutafuta maji.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: MKUU WA MKOA AZINDUA MIRADI YA MAJI KWA AJILI YA VIJIJI VYA SARANDA NA SUKAMAHELA NA KUPIGA MARUFUKU BIASHARA YA MKAA WILAYANI MANYONI. Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top