728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Tuesday, September 13, 2016

  Kibaha yatoa msaada wa milioni 5 kwa vijana waliosomeshwa chini ya mradi wa YEE  Mratibu wa Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) Kanda ya Mashariki, Adolf Jeremiah akiongea na waandishi wa habari juu ya maendeleo ya vijana hao baada ya kuhitimu mafunzo ya ufundi katika Chuo cha Elimu na Ufundi Stadi (VETA), mradi huo unafadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya na kuratibiwa na Shirika la Plan International.
   

  Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Kibaha.

  Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha imewasaidia vijana waliopitia katika mradi wa kuendeleza Vijana Kiuchumi (YEE) kwa kuwapa jumla ya shilingi milioni 5 kwa ajili ya kuwawezesha kujisajili katika vikundi mbalimbali vitakavyowasaidia kuendeleza kazi zao.

  Msaada huo umetolewa hivi karibuni baada ya vijana hao kuhitimu mafunzo ya ufundi yaliyokuwa yakiendeshwa na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Pwani na kutakiwa kuunda vikundi kulingana na fani walizosomea ili kuweza kujisajili katika vyama hivyo vitakakavyowawezesha kupata fursa mbalimbali.

  Hayo yamesemwa leo wilayani Kibaha na Afisa Maendeleo ya Vijana wa Wilaya hiyo, Yahaya Mbogolume alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari hii juu ya maendeleo ya vijana hao baada ya kuhitimu mafunzo ya fani mbalimbali chini ya mradi huo.

  Mbogolume amesema kuwa mradi huo umekuja wakati muafaka kwani umekuwa chachu ya maendeleo ya Halmashauri hiyo kwa sababu asilimia kubwa ya wakazi wa eneo hilo ni vijana ambao walikuwa hawana cha kufanya lakini kupitia fursa hiyo vijana wameweza kujiajiri.

   “Hawa ni vijana wetu wako kwenye eneo letu hivyo, sisi kama Halmashauri ni wajibu wetu kuhakikisha wanajiajiri na kuweza kupata kipato , kwa kutambua hilo tumetoa shilingi milioni 5 kwa ajili ya kusaidia vijana waliopo kwenye mradi wa YEE kujisajili kwenye vikundi vitakavyowasaidia kuongeza vipato vyao”, alisema Mbogolume.

  Afisa huyo ameongeza kuwa Halmashauri inaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwapa mikopo inayowasaidia kuendeleza biashara zao ambapo kwa mwezi huu halmashauri hiyo imetenga jumla ya shilingi milioni 8 kwa ajili ya kuwaendeleza kiuchumi vijana hao ambao wameonyesha uhitaji baada ya kupata mafunzo ya ufundi wa fani mbalimbali.

  Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa YEE Kanda ya Mashariki, Adolf Jeremiah amesema kuwa mradi huo hautoishia kuwapatia ujuzi tu bali utaendelea kuwawezesha kichumi ili kuhakikisha vijana hao wanasimama imara na wanapata maendeleo kupitia fani walizozisomea.

  “Shirika la Plan International tumeamua kusaidia vijana kwa hali na mali hivyo ni lazima kuhakikisha wanayafikia malengo yao, kwa sasa tumewasiliana na VETA wafanye tathmini ya vifaa vinavyotakiwa na vijana hao ili tuweze kuvinunua na kuwagawia waendeleze fani zao zinazowasaidia katika maisha yao ya kila siku”, alisema Jeremiah.

  Naye mmoja wa wahitimu wa mradi huo, George Geligoali ametoa rai kwa vijana wenzie kuacha kudharau fursa zinazotolewa na makampuni mbalimbali na badala yake wazichangamkie kwa kuwa fursa hizo ni kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kiujumla.

  Amelishukuru Shirika hilo kwa kumuwezesha kupata mafunzo katika fani ya umeme ambayo inampatia kipato kinachomuwezesha kujikimu yeye na kuhudumia wazazi wake.

  Katika Halmashauri hiyo, jumla ya vijana 355 waishio kwenye mazingira magumu wameshahitimu mafunzo ya ufundi katika awamu ya kwanza na ya pili ya mradi, vijana 188 wanaendelea na mafunzo ya awamu ya tatu. Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Kibaha yatoa msaada wa milioni 5 kwa vijana waliosomeshwa chini ya mradi wa YEE Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top