728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Sunday, September 11, 2016

  Dumisheni Michezo kuongeza ufanisi katika kazi; Katibu Mkuu Kiongozi.

  Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi
   Na Shamimu Nyaki WHUSM. 

  Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amewataka Watumishi wa Umma kushiriki katika Michezo mbalimbali ili kuwa na afya imara itakayosaidia ufanisi katika kutekeleza kazi zao. 

  Balozi Kijazi ametoa rai hiyo leo Jijini Dar es Salaam katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi Dk.Lawrence Ndombaro katika Bonanza la Michezo la ufunguzi wa mashindano ya thelatini na nne yanayojulikana kama SHIMIWI lililofanyika katika Uwanja wa Uhuru wa Jijini humo. 

  “Michezo inasaidia mwili kuwa na afya njema na kuondoa msongo wa mawazo pamoja na kuleta nguvu na akili katika mwili vinavyosaidia katika utendaji bora wa Mtumishi kwa maendeleo ya Taifa”.Alisema Balozi Kijazi.
  Aidha Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Kijazi amewataka Viongozi wa Serikali na Taasisi zake kutenga muda kwa Watumishi wanamichezo wa kufanya mazoezi pamoja na kuwapatia vifaa vya michezo ili waweze kufanikiwa katika mashindano hayo. 

  Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel amewapongeza Watumishi wake kwa kushiriki Bonanza hilo na kuahidi kuwapa muda mzuri wa maandalizi ili wafanye vizuri katika mashindano hayo. 

  Akifafanua maandalizi ya timu ya Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Mwenyekiti wa timu hiyo Bw. John Manyika ameahidi ushindi kwa timu yake kwani wanaendelea kijiandaa vizuri katika mazoezi. 

  Mashindano ya SHIMIWI yanatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu mjini Dodoma kuanzia tarehe 14 ikiwa ni kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kmbarage Nyerere. 

  Bonanza hilo lilimalizika kwa timu ya Jiji la Dar es Salaam kutwaa Kikombe kwa kuwa na wanamichezo wengi ikifuatiwa na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Dumisheni Michezo kuongeza ufanisi katika kazi; Katibu Mkuu Kiongozi. Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top