728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Tuesday, September 20, 2016

  CCM ZANZIBAR YAPIGA MSASA WAWAKILISHI

  Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar


  Na Is-haka Omar, Zanzibar.

  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka Wawakilishi, Wabunge na Madiwani wa Chama hicho kujenga utamaduni wa kutoa taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kila baada ya miezi mitatu ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji.

  Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar, Vuai Ali Vuai alipokuwa akizungumza na Kamati ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaotokana na CCM Zanzibar huko Afisini Kwake Kisiwandui Mjini hapa.

  Alisema viongozi hao wamekuwa wakifanya kazi mbali mbali za kimaendeleo ambazo ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya CCM, lakini zimekuwa hazijulikani kwa baadhi ya wananchi na viongozi wa Chama kutokana na kutofuatwa utaratibu wa kutoa taarifa rasmi kila baada ya miezi mitatu ili zijadiliwe na ngazi husika kama ibara ya 189 ya ilani ya CCM inavyoelekeza.

  Vuai aliwakumbusha Viongozi hao kwamba licha ya majukumu waliokuwa nayo katika vyombo vya kutunga sheria bado wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanawatumikia wananchi kwa ufanisi katika kupunguza kero na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.

  “Nakukumbusheni kwamba suala la kutoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM katika majimbo yenu ni muhimu sana kwani ndio kipimo cha utendaji wenu kwa wananchi, na hatua hiyo itatoa fursa kwa viongozi mbali mbali wa chama kuhoji ni kwa namna gani kila kila kiongozi anatekeleza wajibu wake kwa wananchi na chama kwa ujumla.”

  Kwani hata kwa upande wa Chama Makao Makuu tunatoa taarifa mbali mbali za utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa upande wa Zanzibar Makamo wa Pili wa Rais anatoa taarifa na upande wa Tanzania bara Waziri Mkuu atatoa taarifa ili kujua Chama na Serikali wamefanya nini kwa wananchi na zinajadiliwa na kuhojiwa,”, alieleza Vuai na kuongeza kuwa endapo viongozi hao watashirikiana kikamilifu wataweza kupunguza kwa haraka changamoto zinazowakabili wananchi Majimboni.

  Alieleza kwamba viongozi hao waliochaguliwa na wananchi, wanatakiwa katika utekelezaji wa Majukumu yao kuhakikisha wanawashirikisha Viongozi wa Chama wa ngazi mbali mbali ili waweze kutathimini na kuweka kumbukumbu za kazi hizo kwa usahihi.

  Alisema kila kiongozi aliyetokana na CCM anatakiwa kuendelea kuongozwa na dhana ya ushindani wa maendeleo ndani ya jimbo lake ili aweze kuaminiwa na wananchi waliomchagua.

  Naibu Katibu Mkuu huyo, alieleza kuridhishwa kwake na kasi ya kiutendaji ya baadhi ya viongozi wakiwemo wawakilishi, wabunge na Madiwani katika maeneo yao na kuwasihi kuendelea kujituma ili kutengeneza tiketi halali ya kuaminiwa na wananchi waliowapa dhamana za uongozi.

  Sambamba na hayo aliwasihi kujenga utamaduni wa kufanya ziara za mara kwa mara katika maeneo mbali mbali yaliyopo katika majimbo yao ili kubaini changamoto sugu zinazowakabili wananchi ili zipatiwe ufumbuzi kwa haraka.

  Alisema viongozi wa Chama hicho, wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa kila sekta kwani kufanya hivyo ndio taswira halisi ya ukomavu wa kisiasa wa CCM.

  Aidha aliwapongeza Wajumbe hao wakiwemo Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwa juhudi zao za kufanya kazi kwa bidii katika kuwaletea wananchi maendeo katika Nyanja mbali mbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

  Alifafanua kwamba kasi ya utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho kwa baadhi ya majimbo inaongeza faraja kwa wananchi hasa katika juhudi za kuomarisha miundo mbinu mbali mbali ikiwemo Ujenzi wa vituo vya afya na ununuzi wa dawa na ununuzi wa gari za wagonjwa.

  Kwa upande wa sekta ya elimu alizitaja juhuzi za viongozi hao kwamba wameweza kuimarisha mabanda (madarasa) na kununua bati za kuezekea sambamba na kununua madawati ili kuwasaidia wanafunzi wakae katika mazingira bora.

  Akizungumzia sekta ya Miundombinu ya Barabara na Maji alisema baadhi ya viongozi wameweza kutengeneza barabara za ndani na kushirikiana na serikali kufikisha huduma za maji kwa wananchi.

  Sambamba na hayo amewashauri viongozi hao kuhakikisha wanashiriki kikamilifu vikao vyote vya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Bunge, kwani kupitia vikao hivyo ndio wataweza kuwasilisha, kuhoji, kushauri na kuitaka serikali kutatua kwa haraka changamoto zinazowakabili wananchi.

  Pamoja na hayo Naibu Katibu Mkuu Vuai aliwambia viongozi hao kwamba kwa yeyote atakayetaka ushauri na muongozo wa jambo lolote la kichama, Afisi yake ipo tayari kumuunga mkono wakati wowote ili kuhakikisha kazi na majukumu waliopewa na wananchi yanafanyika kwa ufanisi zaidi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: CCM ZANZIBAR YAPIGA MSASA WAWAKILISHI Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top