728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Wednesday, August 3, 2016

  Utumishi yapokea vijana wa kujitolea kutoka Japani  Serikali ya Tanzania inadhamini mchango mkubwa unaotolewa na Serikali ya Japani kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA) ambalo limekuwa likishirikiana na Serikali katika kazi mbalimbali za maendeleo hapa nchini.

  Naibu Katibu Mkuu , Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Susan Mlawi alisema hayo mapema leo katika ukumbi wa mikutano wa Utumishi wakati wa hafla fupi ya kuwakaribisha watalaam wa kujitolea kutoka Japani.

  “Tangu mwaka 1967 hadi sasa zaidi ya vijana wa Japani 1,500 wameshafika nchini na kufanya kazi za kujitolea katika maeneo mbalimbali hata katika mazingira magumu” Bi. Mlawi alisema na kuongeza kuwa kunufaika huko kwa Tanzania kunatokana na ushirikano baina ya Serikali ya Japani na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

  Alisema Tanzania itaendelea kudumisha ushirikiano huo na Japani ili kuendelea kunufaika hasa katika suala zima la kujengewa uwezo katika sekta ya elimu na maendeleo ya jamii , sekta ambazo pia zimepewa kipaumbele katika Awamu ya Pili ya Mpango wa Serikali wa miaka Mitano (5) wa Maendeleo inayoanza mwaka 2016/17 na kumalizika mwaka 2021 /22.

  Kwa upande wake, mwakilishi mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo Japani (JICA) nchini Tanzania Bw. Toshio Nagase alisema wataalam hao ambao wako sita (6) watafanyakazi ya kujitolea katika sekta ya elimu kwa miaka miwili na kwa kipindi hicho wanaamini Watanzania watakuwa wamenufaika na ujuzi toka kwa vijana hao.

  Alisema watajitolea kufundisha masomo ya Sayansi, Hisabati, Masuala ya Maendeleo ya Jamii na Michezo katika shule za Sekondari , Shule za Msingi na Ofisi za Maendeleo ya Jamii katika Mikoa ya Morogoro, Pwani , Mtwara , Dodoma na Dar es salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Utumishi yapokea vijana wa kujitolea kutoka Japani Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top