728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Monday, August 29, 2016

  Serikali kuanza kupima utendaji kazi kwa Taasisi za Umma

  Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO - Dar es Salaam

  Serikali imejipanga kuanzisha mikataba ya utendaji kazi kwa Taasisi za Umma katika mwaka ujao wa fedha kwa ajili ya kuhakikisha watumishi hawafanyi kazi kwa mazoea.

  Kauli hiyo imetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki alipokuwa akifanya mahojiano kwenye kipindi kinachorushwa na TBC1 cha ‘TUNATEKELEZA’ kinachoelezea utekelezaji wa mipango na mikakati iliyowekwa na Wizara yake katika kipindi cha Uongozi wa Awamu ya Tano.
  Mhe. Kairuki amesema kuwa kwa kawaida Watumishi wa Umma hupimwa utendaji kazi wao kwa kujaza fomu za wazi zijulikanazo kama ‘OPRAS’ lakini upimwaji huo hauonyeshi utendaji wa Taasisi nzima,  hivyo ili kufahamu mipango na malengo ya Taasisi ni lazima kuwe na upimaji wa utendaji kazi wa Taasisi nzima.
  “Sisi kama Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma tumeona kuna haja ya kuwa na mikataba ya kupima utendaji kazi wa Taasisi husika ,tumeshakamilisha maandalizi na kila kitu kikienda salama mwaka ujao wa fedha tutaanza zoezi hili”, alisema Mhe. Kairuki.
  Waziri huyo ameongeza kuwa zoezi hilo limeshindikana kuanza mwaka huu wa fedha kwa kuwa bado maandalizi yake hayajakamilika na kuongeza kuwa taasisi zote zinatakiwa kupewa mafunzo kabla ya kusaini mikataba hiyo.
  Amefafanua kuwa Serikali itaingia makubaliano kwa taasisi husika kwa kufuata ngazi za uongozi kuanzia kwa Mkuu wa Taasisi hadi kwa kiongozi wa juu kabisa wa Wizara husika.
  Aidha, Mhe. Kairuki amewakumbusha Watumishi wa Umma kuwa kuvujisha nyaraka za Serikali ni kosa la jinai hivyo kila mtumishi anatakiwa kuzingatia kanuni za kudumu za Utumishi wa Umma ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa nidhamu na uwajibikaji wa hali ya juu.
  “Sheria ya Usalama wa Taifa na Sheria inayosimamia masuala ya kumbukumbu za nyaraka Serikalini inasema wazi kuwa ni kosa la jinai kuvujisha nyaraka za Serikali kwahiyo natumia fursa hii kukemea mtu yeyote mwenye tabia hiyo kwa sababu hatua kali zitachukuliwa dhidi yake”, alimalizia Mhe. Kairuki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Serikali kuanza kupima utendaji kazi kwa Taasisi za Umma Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top