728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Sunday, August 21, 2016

  RC NDIKILO AWASIMAMISHA MAAFISA ARDHI WAWILI IDARA YA ARDHI MKURANGA

   
  Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, mwenye kifimbo akionyeshwa na baadhi ya maafisa ardhi ,ramani ya eneo linalomilikiwa na mmiliki Youth with A mission shamba namba 1691 huko Mwandenge ambalo heka 30 imemegwa kwa ajili ya kupatiwa kampuni ya bakhresa food products pasipo uongozi wa halmashauri kujulishwa mchakato unavyokwenda(picha na Mwamvua Mwinyi) 

  Na Mwamvua Mwinyi,Mkuranga

  MWENYEKITI wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,amewasimamisha kazi mara moja,maafisa ardhi wawili wa halmashauri ya wilaya ya Mkuranga kutokana na kutumia vibaya ofisi hiyo.

  Mwenyekiti huyo amemsimamisha kazi afisa ardhi mteule wa halmashauri hiyo Riziki Chagie na afisa ardhi Mussa Kichumu ili kupisha uchunguzi utakaofanywa na taasisi ya kudhibiti kupokea na kutoa rushwa(TAKUKURU) na vyombo vingine vya dola. Aidha amelielekeza Jeshi la polisi kuwakamata mara moja ,watumishi hao na kuwaweka ndani ili hatua nyingine ziweze kufuata mkondo wake.

  Aidha mhandisi Ndikilo,ameiagiza TAKUKURU chini ya mkuu wa taasisi hiyo mkoa Susan,ihoji mchakato mzima uliowashirikisha watumishi hao .Na kuangalia nyaraka upya na mazingira yaliyowafikisha kumega ardhi ya mmiliki halali Youth with A mission shamba namna 1691 pasipo kushirikisha uongozi wa halmashauri.

  Sambamba na hayo ameitaka taasisi hiyo kuhoji wale wote ambao kwa namna moja ama nyingine walishiriki katika mchakato huo ndani ya halmashauri hiyo ambapo atatoa nyaraka na vithibitisho kwa ajili ya uchunguzi. Ameeleza kuwa endapo uchunguzi huo utabaini kuna mtumishi ameshiriki , ametumia ofisi yake vibaya ama ushauri wowote wa kijinai basi sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho kwa watumishi wengine.

  Mhandisi Ndikilo ambae pia ni mkuu wa mkoa wa Pwani,aliyasema hayo wakati kamati ya ulinzi na usalama mkoa ilipokwenda kufuatilia taratibu zilizotumika kumegwa hekari 30 katika shamba namba 1691 lililopo Mwandege na kupewa kampuni ya Bakhresa food products kwa kiasi cha sh.mil 458.

  Sambamba na hayo alimuagiza katibu tawala mkoani humo(RAS)Zuberi Samataba, kutenga fedha za kuhamisha watumishi wengine idara ya ardhi katika halmashauri hiyo kwani waliopo wanadaiwa kugeuza ofisi hiyo kitega uchumi kwa maslahi yao binafsi.

  Mhandisi Ndikilo alisema,kamati ya ulinzi na usalama mkoa iliketi na kupitia nyaraka zote baada ya kumuagiza mkuu wa wilaya kupeleka taarifa ya wilaya ,taarifa ya kutoka kwa mmiliki wa shamba hilo. Kamati hiyo pia iliihitaji taarifa ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo,taarifa ya afisa ardhi mteule wa ardhi na kisha walijadiliana kwenda kutembelea eneo husika na kukaa pamoja baina ya pande zote.

  Alisema kamati ya ulinzi na usalama mkoa, ililazimika kwenda kufuatilia taarifa iliyoipata kuhusu kumegwa kwa heka 30 za shamba la Youth with A mission na kugawiwa kwa kampuni ya bakhresa food products ambae amelipia kiasi cha sh .mil 458 pekee ikiwa ni katika mchakato wenye mazingira ya kutatatanisha. Kamati hiyo ilishangazwa kampuni hiyo kutoa gharama ya mil.458 wakati kwa thamani ya heka 30 kwasasa ingekuwa atoe bil.4.749 ambazo zingeweza kutumika katika matumizi mbalimbali ya jamii ikiwemo kujengea madarasa,stend,shule ama kununulia madawati .

  Mhandisi Ndikilo alieleza kuwa watumishi hao wapo chini ya serikali na halmashauri lakini walikuwa vinara wakubwa kusimamia mchakato huo. “Katika barua ya halmashauri baada ya kamishna wa ardhi kuanza kuhoji juu ya shamba hilo kuna barua ilisainiwa na R.M .Chagie,barua ya tr 8,feb 2016 kwa niaba ya mkurugenzi ,kichwa cha habari cha habari kikisema ombi la kampuni ya bakhresa kumilikishwa shamba namba 1691”

  “Barua ya mtumishi huyo alimalizia na kumshauri kamishna kwamba shamba hilo lenye hekari 81,linalomilikiwa kihalali na hati ni mmiliki halali Youth with A mission na ni vigumu kugawiwa kwa mmiliki mwingine labda kama litatwaliwa kwa manufaa ya umma na fidia stahili kwa kufutwa sheria zote’alinukuu . Inasema ni vema muombaji huyu bahkresa ashauriwe kuwasiliana na mmiliki ili kufanya mapatano binafsi na wizara ihusike katika kufanya uhamisho wa umiliki pekee.

  Afisa mteule aliyesimama kwa niaba ya halmashauri baada ya kuwasilisha taarifa hiyo ,kamishna msaidizi wa ardhi kanda ya mashariki na timu yake ilikwenda Mkuranga tr 5 may mwaka huu kuthibitisha taarifa hiyo na kuambatana na maafisa ardhi wa Mkuranga na kufanya ukaguzi na mahojiano na mkurugenzi wa taasisi hiyo Jeremiah Kiwinda.

  Nae Musa Kichumu kwa niaba ya mkurugenzi aliandika baada ya ukaguzi huo,timu hiyo imeagiza kupatikana kwa uthibitisho wa uraia wa mkurugenzi wa taasisi hiyo na nakala halisi wa umiliki,miktasari ya kijiji,nakala halisi ya ramani na mipango miji. Kisha ilikuja barua iliyoambatanishwa na barua ya ombi la bakhresa kuomba eneo katika shamba hilo,na barua nyingine kutoka wizara husika inayosema kuna uendelezaji wa shamba hilo na umiliki ni halali hivyo eneo limegwe kwa kuanzia heka 3 kwa matumizi ya soko la umma.

  Mhandisi Ndikilo alisema, mchakato mzima hauna maslahi mapana kwa halmashauri wala wilaya bali kwa nutunisha mifuko kwa baadhi ya watumishi. Alielezea kuwa wamesitisha mchakato huo unaoendelea kutokana na watumishi hao kuubeba na kuwa vinara wakubwa bila ya kuushirikisha uongozi wa halmashauri wala wilaya. Mhandisi Ndikilo,alipeleka salamu maalumu kwa watumishi wasio waadilifu na wanao vuruga taratibu za kazi, kujitafutia kipato kinyume na sheria na kuacha kushirikisha viongozi wao wa kazi ,kuwa wataishia katika utaratibu huo .

  Alimtaka mkurugenzi wa halmashauri ya Mkuranga,kusiamamia watumishi wake na kuchukua hatua kwani mamlaka anayo kwa kufuata sheria . Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Juma abeid alisema walikuwa hawakushindwa kutatua jambo hilo, kutokana ni dogo kwao hivyo ameishangaa kamati ya ulinzi na usalama mkoa.

  Kufuati kauli hiyo mhandisi Ndikilo,alimwambia suala hilo sio jepesi kama anavyofikiria na kumuonya kuacha tabia ya kuzungumza maneno ya mzaha kwenye mambo mazito. Mhandisi Ndikilo alisema kutokana na kauli hiyo ndio inazidi kuwatia shaka kwani serikali ya mkoa haifanyikazi kwa kukurupuka wala kubahatisha.

  “Hii ni wikendi ,tupo hapa kwani hatuna kazi za kufanya,usiwe mwepesi wa kuongea mambo bila kufikiria,kwahili unanipa wasiwasi ,naomba uache kamati na vyombo vya usalama vifanye kazi yake”alisema mhandisi Ndikilo. Mkurugeni wa Youth with A mission ,Jeremiah Kiwinda ,alisema hakupewa nafasi na kushinikizwa kumega hekari 30 kwa ajili ya kupewa bakhresa food products na mipango ataitekeleza haikusikilizwa.

  Kiwinda alisema wakati wanaanzisha taasisi hiyo walipitia ngazi ya kijiji,wanatambulika wilayani,wamesajiliwa na kumiliki eneo kihalali tangu mwaka 1992 na kusajiliwa rasmi mwaka 1999. Mkurugenzi wa halmashauri ya Mkuranga,Injinia Munde Mshamu ,alieleza mchakato uliokuwa ukifanywa na watumishi hao unatia shaka hivyo ameusimamisha hadi atakapojiridhisha.

  Alisema hatua ya ufuatuatiliaji,kuanzia mchakato wa ramani,barua zakuhoji inatia mashaka makubwa kwani taarifa iliyowasilishwa na afisa ardhi mteule Chagie na afisa ardhi Musa ilipaswa ifuate hadidu rejea alizowapa akiwa kama mkuu wao wa kazi. Alisema watumishi hao wamekuwa wakitumia nafasi walizonazo na kuvuka nafasi za wengine ambao wangeshirikiana ikiwemo vikao vya madiwani,mkurugenzi na idara ya fedha ambayo ilikuta fedha imeingizwa bila kujua ilipotoka .

  Injinia Mshamu alisema suala hilo limeenda kiharaka bila kufuata taratibu za vikao ya kulijadili na badala yake limepelekwa haraka kwa kusimamiwa na watumishi wawili wa idara ya ardhi pasipo kushirikishwa. Nae mbunge wa jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega alimshukuru mkuu wa mkoa kwa kuwa karibu kufuatilia na kusimamia masuala nyeti kama hayo.

  Alikana kuhusiaka na kupanga kiwango cha fedha alicholipishwa kamapuni ya Bakhresa food products kama inavyodaiwa. Ulega anasema anajua thamani ya hela na anajua pesa hivyo hawezi kuhusiaka kwa hilo ambapo amelijua likiwa katika hatua za mwisho.

  Alisema wakati aliposiki halmashauri imepata fedha kwa mujibu wa sheria ndipo aliposhukuru kupatikana kwa fedha hiyo mil. 458.Shamba namba 1691 lililopo Mwandege ,mali ya taasisi ya Youth with A mission,linamilikiwa kihalali zaidi ya miaka 15 iliyopita na kuendeleza hekari 24 kati ya hekari 81 zilizopo,ambapo kupitia halmashauri iliomba hekari 3 kwa ajili ya ujenzi wa soko ambapo ilipewa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: RC NDIKILO AWASIMAMISHA MAAFISA ARDHI WAWILI IDARA YA ARDHI MKURANGA Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top