728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Friday, August 26, 2016

  MHE. AUGUSTINO MREMA APONGEZA UTENDAJI KAZI WA SERIKALI YA AWAMU YA TANO YA RAIS DKT. JOHN MAFUGULI

   Mh.Mrema.
   
  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepongezwa kwa hatua yake ya kurejesha maadili na miiko ya utumishi kwa watumishi wa umma nchini hali iliyosaidia kurejesha uwajibikaji wa Serikali kwa wananchi.

  Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Misamaha kwa Wafungwa (PAROLE) na Mbunge wa Zamani wa Jimbo la Vunjo, Mhe. Augustino Mrema wakati wa mahojiano yake maalum na mwandishi wa habari hii akieleza kuhusu mafanikio ya mipango na mikakati mbalimbali ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

  Mrema alisema tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu Tano, kumekuwepo na mabadiliko kwa watendaji wa umma katika ngazi mbalimbali za kimamlaka ukitofautisha na miaka ya nyuma ambapo baadhi ya watendaji walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea.

  “Viongozi wengi wa umma walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea bila kujali wajibu wao na wala hakukuwa na uwajibikaji cha kusikitisha mamlaka husika zilikuwa haziwachukulii hatua za kinidhamu, hivyo viongozi wa umma badala ya kuwatumikia wananchi wakawa wanatumikia matumbo yao” alisema Mrema.

  Kwa mujibu wa Mrema alisema Rais Magufuli ameanza kutekeleza kwa vitendo ahadi yake aliyoitoa kwa wananchi ya kuwaondoa madarakani viongozi wazembe na wasiowajibika na wasiokuwa na uwezo wa kufanya kazi katika kuwatumia wananchi.

  Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inastahili pongezi kwa hatua inazochukua katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi ikiwemo uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi nchini, kwani hakuna maendeleo yatakayoweza kupatikana katika nchi pasipo na kupiga vita rushwa.

  Mrema alisema ni wajibu wa kila mwananchi kuichukia rushwa kwa vitendo ikiwemo kuwafichua hadharani kikundi cha watu kinachojihusisha na rushwa kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia Tanzania kupiga hatua kubwa za maendeleo.

  “Kama mnavyokumbuka mimi nilifukuzwa kazi serikalini kwa sababu ya kupinga ufisadi ambao kwa wakati ule ulikuwa umekithiri serikali, ivyo nilichokuwa nikikipigania mimi ndicho anachifanya Rais Magufuli” alisema Rais Magufuli.

  Wakati huo huo , Mhe. Mrema amesema kuwa hakuna haja ya kufanya maandamano Septemba Mosi kwani hayana faida yoyote kwa taifa badala yake wananchi wa kawaida ndio watakaoathirika.

  Amewasihi wananchi kutumia muda huo kufanya shughuli nyingine za maendeleo badala ya kuandamana kwa kuwa hakuna demokrasia isiyo na mipaka. “Mikutano ya hadhara na maandamano yasiyokwisha kila kukicha yatasababisha wananchi wasifanye kazi. Nchi yetu ni maskini hivyo tunahitaji wananchi wafanye kazi kwa bidii” alisema Mrema.

  Aliwataka Watanzania kukumbuka maandamano ya mwaka 2001 yaliyoitishwa na Chama cha Wananchi (CUF) huko Zanzibar ambapo watu kadhaa waliuwawa na mamia kukimbilia uhamishoni nchini Kenya na Somalia.

  Akifafanua zaidi Mrema alisema kuwa iwapo CHADEMA wataona wameonewa ni vyema watumie njia za mazungumzo au ikibidi kwenda mahakamani badala ya kufanya maandamano ambayo yanaweza kusababisha vurugu na kuharibu amani na utulivu wa nchi.
   
  Na Ismail Ngayonga
  MAELEZO
  Dar es Salaam
  25.8.2016
   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: MHE. AUGUSTINO MREMA APONGEZA UTENDAJI KAZI WA SERIKALI YA AWAMU YA TANO YA RAIS DKT. JOHN MAFUGULI Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top