KASI ya Rais
Magufuli katika kuhakikisha Tanzania inajitegemea kwa kila mhusika kulipa kodi
imeanza kulipa kufuatia takwimu kuonesha kwamba watalii wameongezeka nchini na
hivyo kuongeza mapato zaidi Serikalini.
Ukweli huo
umetolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof Jumanne
Mghembe alipokuwa akizungumza kuhusu mikakati mbalimbali iliyotekelezwa na Wizara yake.
“Pamoja na
kelele za sekta ya utalii baada ya Serikali kuanza kutoza Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT) katika sekta ya utalii, lakini nakuhakikishia hivi sasa watalii
wameongezeka nchini na mapato yamekua kwa asilimia 22 zaidi,” alisema Waziri
Maghembe.
Waziri Maghembe
ametanabaisha kuwa tofauti na mtazamo wa wadau wa sekta ya utalii ongezeko la
kodi hiyo halijaathiri watalii wengi hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania inabaki
kuwa na vivutio vya kipekee duniani.
“Nchi yetu ina
vivutio vingi ambavyo havipo nchi nyingine yoyote. Hii ikijumlishwa na hali ya
amani na utulivu iliyopo nchini, hakuna mtalii atakayeshindwa kugharamia
ongezeko la dola nane tu,” alisema Waziri Maghembe.
Alitumia muda
huo pia kueleza kuwa utafiti wake katika nchi za nje unaonesha kwamba Balozi za
Tanzania zinaongoza kutoa viza kwa watalii mbalimbali ikilinganishwa na nchi
nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki hasa katika miji mikubwa kama Berlin.
Akizungumzia
vita dhidi ya ujangili, Waziri Maghembe amesema juhudi za Serikali kuwekeza
katika mafunzo na vifaa vya kisasa zimezaa matunda pia baada ya ujangili kupungua nchini kwa kiasi kikubwa.
Alisema tayari
watuhumiwa wakubwa wa mtandao wa ujangili wameshakamatwa na baadhi wamehukumiwa
vifungo jela. Alimtaja mmoja wa watuhumiwa wakubwa wa mtandao huo raia wa
kigeni ajulikanaye kwa jina la “Malkia wa Pembe za Ndovu” naye yuko mahabusu
kwa sasa.
“Katika vita hii
tumeamua kuuchukulia ujangili kama ugaidi au uhujumu uchumi. Tumekamata
majangili wakubwa na wafadhili wao na bado vigogo zaidi tunaendelea
kuwafuatilia na muda wowote tutawakamata,” alisema.
Aliongeza kuwa
Serikali pia imepiga marufuku uvunaji wa mazao ya misitu hasa magogoro bila
leseni na kwamba atakayefanya hivyo atakamatwa, mali na gari husika
vitataifishwa na wahusika kufikishwa mahakamani.
Takwimu za
kuongezeka watalii nchini zinaipa nguvu Serikali ya Rais Magufuli kwa sababu
tangu alipoingia amekuwa akisisitiza sana katika umuhimu wa kukusanya kodi ili
nchi ijitegemee. Tofauti na mtazamo huo, baadhi ya watu wamekuwa hawaamini kama
hilo linawezekana.
0 comments:
Post a Comment