728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Monday, August 22, 2016

  ASASI ZENYE MWELEKEO WA KUSHABIKIA USHOGA, KUKIUKA MAADILI KUWAJIBISHWA


  Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) na Naibu Katibu Mkuu Bw. Amon Mpanju (wa tatu kulia) baada ya kumaliza kikao jijini Dar Es Salaam.
  Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe akiongea katika kikao na watendaji wa Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) walipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

  Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe amezitaka asasi za kiraia zisiyumbishwe na misaada toka nje yenye mwelekeo wa kukinzana na mila, desturi, utamaduni, imani za Watanzania, sheria na Katiba ya nchi.

  Mhe. Dkt Mwakyembe ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam alipokutana na uongozi wa Taasisi ya Mtandao wa Jinsia Nchini (TGNP) ofisini kwake na kuwaambia kuwa Serikali inaunga mkono juhudi za asasi mbalimbali za kiraia kama vile TGNP za kuelimisha jamii na kutetea haki za watoto, wazee, wanawake, walemavu na makundi mengine maalum yanayostahili fursa na haki sawa katika jamii yetu lakini haitazivumilia asasi ambazo zinaenda kinyume na maadili ya nchi na kukiuka sheria na taratibu ambazo kama nchi imejiwekea.

  “Serikali inaunga mkono kazi zinazofanywa na asasi za kiraia nchini lakini niweke wazi kuwa hatutazivumilia asasi za kiraia zinazoyumbishwa na misaada toka nje na kujihusisha na vitendo ambavyo vinakiuka maadili, taratibu na sheria za nchi ambazo zipo kwa mujibu wa sheria,” alisema Mhe. Waziri.

  Alitolea mfano wa mashinikizo hayo kutoka kwa nchi zenye nguvu kiuchumi duniani kama ya kutaka nchi zinazoendelea au asasi zikubali ushoga na ndoa za jinsia moja kama sehemu ya haki za binadamu kama njia ya kuendelea kupata misaada kutoka kwao na kuongeza kuwa asasi zenye muelekeo huo nchini zinachunguzwa na zitakazobinika zitachukuliwa hatua kali.

  "Nchi hizo zimekuwa zikitoa mashinikizo kwa nchi zetu na hasa asasi nyingi zikizitaka zikubali ushoga na ndoa za jinsia moja, tunazichunguza asasi zote za kiraia zenye mwelekeo huo na tukibaini mapungufu hayo tutazichukulia hatua kali za kisheria, uchafu na upuuzi huo wa Wazungu, ubaki hukohuko kwao," alisisitiza.

  Waziri Mwakyembe alionya kuwa nchi ikilegeza kamba katika suala hili, tutashinikizwa baadaye kufunga ndoa na wanyama wa kufugwa kwamba nayo ni sehemu ya haki za binadamu.

  Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Amon Mpanju, alisisitiza umuhimu wa asasi za kiraia kuisaidia Serikali kwa kupeleka kwenye jamii ujumbe sahihi wenye mafundisho badala ya kusubiri kukosoa tu na kuzitaka asasi za kiraia kuacha kuunga kuunga mkono hoja za ushoga kwa kishawishi cha fedha wanazopewa kutoka kwa wafadhili wao
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: ASASI ZENYE MWELEKEO WA KUSHABIKIA USHOGA, KUKIUKA MAADILI KUWAJIBISHWA Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top