728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Wednesday, July 13, 2016

  Watumishi wa Afya watakiwa kuzingatia weledi na maadili ya kazi

  Hussein Makame-MAELEZO

  Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs) yanaongoza kusababisha vifo duniani kwa asilimia 68 ikilinganishwa na magonjwa mingine.

  Tafiti zinaonesha kwamba magonjwa hayo yameongezeka kwa kasi nchini Tanzania ambapo magonjwa ya moyo yanaelezwa kuongezeka kwa asilimia 10 wakati kisukari kikiongezeka kwa asilimia 9.6.

  Kanuni ya magonjwa inasisitiza kujikinga na magonjwa badala ya kusubiri kuyatibu na ndio maana wataalamu wanashauri kuzingatia kanuni za ulaji bora wa chakula na kufanya mazoezi. Matumizi ya teknolojia ya upigaji picha za eksirei ikiwemo radiolojia au nyuroradiolojia ni njia za kisasa zinazotumika katika kutambua na kutibu magonjwa yasiyoambukiza.

  Ili kuhakikisha wataalamu wa sekta ya afya nchini wanakwenda sanjari na mabadiliko ya teknolojia hiyo, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Baraza la Wataalamu wa Radiolojia Nchini (MRIPC) wanaandaa Mkutano wa Pili wa Nyuroradiolojia wa Afrika Mashariki.

  Mkutano huo umeshirikisha Watafiti, Wataalamu wa Tiba ya Kiradiolojia na picha za eksirei kutoka taasisi za afya za nchi za Kenya, Marekani, Uganda, Korea Kusini, Uingereza na wenyeji Tanzania, kujadili Mada kuu inayohusu “Dhima ya Nyuroradiolojia katika kukabiliana na NCDs.”


  Katibu wa Mkutano wa Nyuroradilojia wa Afrika Mashariki Dkt. Mboka Jacob akizungumza na washiriki wa mkutano wa Pili wa Neuroradiolojia unaofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
  Naibu Mkurugenzi wa Elimu Endelevu na Maendeleo ya Taaluma Dkt. Doreen Mloka akizungumza kwenye mkutano huo.
  Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wataalamu wa Radiolojia (MRIPC) Dkt. Jaffer Dhee akieleza majukumu ya baraza hilo katika fani ya Radiolojia nchini na kumkaribisha mgeni rasmi wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
  Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Bakari Kambi, akizungumza na wataalamu wa Radiolojia kufungua mkutano mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto hivi karibuni.
  Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wakimsikiliza Mgeni Rasmi. Picha zote na Hussein Makame-MAELEZO
  Akizungumza kwenye mkutano huo, Mratibu Mkuu wa Mkutano Dkt. Mboka Jacob anasema lengo la mkutano huo ni kuelimishana na kupeana taarifa juu ya dhima ya Nyuroradiolojia katika kukabiliana na NCDs.

  Anasema lengo lingine ni kubadilishana uzoefu juu ya matibabu na tafiti za kitabibu na kuona jinsi taaluma ya Nyuroradiolojia inavyopiga hatua katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

  “Kama tunavyofahamu nchi nyingi za Afrika zinatumia Radiolojia ya jumla, hii inasababisha kupatikana kwa matokeo ya radiolojia yasiyokidhi mahitaji” anasema Dkt. Mboka na kuongeza kuwa:

  “Labda unaweza kujiuliza kwa nini tumejikita kwenye magonjwa yasiyoambukiza, ni jambo linalosikitisha kwamba Afrika ni sehemu inayobeba mzigo mkubwa wa magonjwa hayo”

  Anasema kuwa kwa mujibu wa ripoti ya WHO ya mwaka 2010, nchi za Afrika za Ukanda wa Jangwa la Sahara zinabeba asilimia 70 ya mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza ambayo mengi yanachangiwa na magonjwa yanayoambukiza, magonjwa ya watoto wachanga na ya kina mama.

  Anaongeza kuwa mbali na magonjwa hayo, kuna ongezeko la mzigo wa magonjwa makali kama kiharusi na magongwa ya moyo.

  “Kutokana na mizigo hiyo miwili, ni wakati sasa kuimarisha si tu kusimamia kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza lakini pia kuimarisha uchunguzi wa upigaji picha za kiradiolojia kwa kuwa ni nguzo muhimu katika usimamizi wa mgonjwa.

  Anasema inafahamika kwamba magonjwa yasiyoambukiza yanasababisha ugumu wa aina nyingi katika kuyatibu lakini ugumu wa nyurolojia ni ugumu unaoharibu zaidi.

  Dkt. Mboka anasema kuwa katika dunia ya sasa, teknolojia za kisasa za tiba na mgawanyo wa kazi katika masuala ya tiba, unahitaji utaalamu wa hali ya juu na weledi katika fani ya radiolojia na vifaa vya radiolojia ili kukidhi mahitiji ya tiba ya kisasa.

  Anasema si tu kwamba wakati umefika kuanzisha Kituo cha Radiolojia Kubwa hapa nchini na Afrika Mashariki lakini pia muda umefika kuifanya fani ya Radiolojia kukua sanjari na mambo mingine ya kitabibu katika hospitali za ukanda huo.

  Katika kukabiliana na changamoto hiyo, MUHAS kupitia Idara ya Radiolojia imeanza mchakato wa kutoa Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Nyuroradiolojia na ipo katika hatua za kukamilisha Mtaala wake.

  Anaiomba Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto iwaunge mkono kwa kuwadhamini wanafunzi kwa ajili ya shahada hiyo.

  Makamu Mwenyekiti wa MRIPC Dkt. Jaffer Dhee ambaye ni Mratibu Mwenza wa mkutano huo, anasema lengo la baraza hilo ni kusimamia weledi na utendaji katika matibabu ya eksirei kwa kutambua kwamba matibabu ya eksirei yanakua kwa kasi kuliko inavyofikiriwa.

  Lakini pia anasisitiza wadau wa radiolojia nchini kuzingatia weledi katika utendaji kazi ili kuepuka changmoto za kimatibabu kwa wagonjwa.

  “Vifaa vipya, namna ya matibabu na njia mpya za kutibu kitu kilekile zinabadilika, ikiwa hatutasimamia weledi na utendaji kazi tutawaweka hatarini wagonjwa, hivyo kufikia hatua ya kuhakikisha sote tunatambulika na kusajiliwa”, Dkt. Jaffer anawasisitiza washiriki na kuongeza kuwa:

  “Tunahitaji kutazama utendaji wenu kama unazingatia maadili na nasisitiza kuzingatia afya ya mgonjwa.Je utatumia njia sahihi za upigaji picha au utapiga picha kutimiza matakwa yako ama utakubali kupokea bahashishi ukitambua kwamba kutoa na kupokea bahashishi hairuhusiwi.”

  Dkt. Jaffer anawaomba wataalamu hao kuwa pindi wanapogundua vitendo hivyo vinafanyika wawasilishe taarifa kwenye Baraza ili chombo icho kiweze kuchukua hatua za ndani dhidi ya kitendo hicho.

  Anawasisitizia kuwa kwa vyovyote wanahitaji kufanya kazi kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba matumizi ya radiolojia kitaifa na Kimataifa yanafanyika kwa kiwango kinachokubalika.

  Akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Bakari Kambi anasema maendeleo ya tasnia ya Tiba hususani katika Radiolojia na picha inaibua mahitaji ya kujiendeleza katika elimu na ujuzi unaendana na taaluma hiyo.

  Anasema mada kuu ya mkutano huo imekuja muda muwafaka wakati Tanzania inatekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia ambapo lengo namba 3 (4) linataka ifikapo mwaka 2030, kupungua robo tatu ya vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza kupitia kukinga na kutibu magonjwa hayo na kwa kuhamasisha afya ya akili na ustawi wa jamii.

  “Kwa hiyo Mpango Mkakati wetu wa sekta ya afya unafanya kazi na unazingatia hili lengo mahususi na tunamalizia uboreshaji wa Mkakati wa Kitaifa kuhusu magonjwa yasiyoambukiza.Kwa hiyo mada yenu ipo pamoja na nini dunia inafanya na nini nchi ya Tanzania inafanya.” Anasema.

  Anasema kuwa Wizara inawafadhili wanafunzi katika fani ya utaalamu wa hali ya juu wa masuala mbalimbali ya kiafya ndani na nje ya nchi na anawahakikishia kwamba Serikali itaendeleza ufadhili huo kadri rasilimali zitakaporuhusu.

  Ndipo ukifika muda wa Prof. Bakari kuzungumza kwa nafasi yake ambapo anasema akiwa Mganga Mkuu wa Serikali anawafahamisha wahusika wote wa sekta ya afya nchini kwamba Tanzania inabadilika kwa kasi sana na kwa nafasi yake anashuhudia mabadiliko hayo.

  “Moja ya mabadiliko makubwa ninayoyaona ni kwamba Watanzania kwa ujumla sasa wanajua haki zao na wanataka kuona nyinyi kama weledi mnatoa huduma inayotarajiwa” anasema Prof. na kuongeza kuwa:

  “Hakuna namna ya kufanya kazi yoyote hapa nchini Tanzania bila ya kuhakikisha kwamba mnazingatia weledi na maadili ya kazi yenu na nahitaji mlizingatie hili”

  “Kwa hiyo kuweni makini kweli, tibuni wagonjwa wenu kwa heshima, hakikisheni mnazingatia maadili na hakikisheni sana mnazingatia weledi wa kazi yenu.Tumeelewana jamani? Nakuhakikishieni sitawatetea iwapo hamtakuwa weledi, yaani sitavumilia hilo”

  Anasema jambo la pili ni wajibu wa wataalamu wa tiba kutumia taaluma yao kuishauri Serikali jinsi ya kuboresha huduma za sekta ya afya nchini.

  “Nyinyi ni wataalamu, tumieni utaalamu wenu kuishauri Serikali vipi tutaipeleka hii tasnia mbele, vipi tuwahudumia vizuri zaidi Watanzania, vipi tutawafanya Watanzania wengi zaidi kupata huduma yetu, vipi mtawafanya Watanzania wamudu huduma zenu.”anawakumbusha.

  Prof. Bakari hakuacha kukumbusha majukumu ya baraza la MRIPC, ambapo anataka kuona limeanza mikakati ya kurahisisha mtu yeyote kuwasilisha malalamiko yake na ionekane wazi kuwa hatua zimechukuliwa kwani kwa sasa si rahisi kwa mwananchi kufanya hivyo.

  Naye Naibu Mkurugenzi wa Elimu Endelevu na Maendeleo ya Taaluma Dkt. Doreen Mloka anasema maendeleo ya ujuzi wa wafanyakazi wa sekta ya afya ni muhimu katika kuinua viwango vya kuwajali wagonjwa na kukabiliana na changamoto za Afya nchini Tanzania.

  Hata hivyo, anasema ili nguvu kazi ya Tanzania katika sekta ya afya itimize malengo yake, wanahitajika kwenda sanjari na maendeleo yanayotokea kwenye taaluma zao na fani walizobobea.

  Dkt. Mloka anamnukuu Mwanasayansi Maarufu Albert Einstein anayesema kuwa “aina kubwa ya kichaa ni kufanya jambo kwa njia ileile na namna ileile kwa muda wote na kutegemea matokeo tofauti.”

  Anasema kuhuisha taaluma ya Tiba itaweza kuleta mabadiliko na kusonga mbele katika kufikia malengo ya maendeleo ya Milenia.

  Anaongeza kuwa kuweka nguvu katika kuboresha ujuzi na elimu ni njia muhimu kwa mipango ya nchi ili kuhakiksha kwamba Taifa linafikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia hasa namba tatu ambalo linahusu kuhakikisha upatikanaji wa maisha yenye afya ifikapo mwaka 2030.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Watumishi wa Afya watakiwa kuzingatia weledi na maadili ya kazi Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top