728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Thursday, July 28, 2016

  TUNAZISUBIRI NEC NA ZEC KUIPIGIA KURA YA MAONI KATIBA INAYOPENDEKEZWA

   waziri wa Mambo ya Katiba na sheria Dkt Harrison Mwakyembe akizungumza na Kikosi cha Kupambana na Haki za Mirathi  (KIKUHAMI ) chini ya WiLDAF uliomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam
   Mwenyekiti wa  Kikosi cha Kupambana na Haki za Mirathi  (KIKUHAMI ) chini ya WiLDAF  Bibi Thabita Siwale akizungumza kumshukuru Waziri wa Mambo ya Katiba na sheria Dkt Harrison Mwakyembe walipokutana nae Ofisini kwake jijini Dar es salaam
  Uongozi  wa Kikosi cha Kupambana na Haki za Mirathi  (KIKUHAMI ) chini ya WiLDAF  katika picha ya pamoja na  Waziri wa Mambo ya Katiba na sheria Dkt Harrison Mwakyembe  na katibi Mkuu Prof Sifuni Mchome walipokutana nao Wizarani jijini Dar es salam.

  Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Harrison Mwakyembe amesema Serikali inazisubiri Tume ya Uchaguzi nchini (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanziba (ZEC) zimalize majadiliano yao ili mchakato wa kuipigia kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa ufanyike.

  Mhe. Mwakyembe ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam alipokutana na uongozi wa Kikosi cha Kupambana na Haki za Mirathi (KIKUHAMI ) kilichoko chini ya Chama cha Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika – WiLDAF.

  Amesema zoezi hilo lingekuwa limeshakamilika ila Tume za Uchaguzi ziliona ni bora liahirishwe kwanza ili kupisha zoezi la Kikatiba lililokuwa likiikabili nchi la Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana likamilike na kwamba kukamilika kwa zoezi hilo kunatoa fursa kwa Serikali kuendelea na mpango wake wa kuendesha kura ya maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa ili kupata Katiba Mpya ya Tanzania.

  Aliongeza kuwa Katiba Inayopendekezwa ina vitu vingi sana ambavyo vitasaidia upatikanaji wa haki za wanawake na kuondoa uonevu dhidi yao na hivyo kufanikisha harakati ambazo wadau mbalimbali wa wanawake nchini wamekuwa wakizipigania na hivyo kukamilika wakati Katiba mpya itakapokuwa imepatikana.

  Aidha Mhe. Waziri ameutaka uongozi huo wa KIKUHAMI kupitia WiLDAF kuwasilisha Wizarani mapendekezo yao juu ya mabadiliko ya sheria mbalimbali za Mirathi nchini wanazoziona zinawakandamiza wanawake ili ziweze kufanyiwa marekebisho na ziendane na wakati uliopo.

  “si mnataka sheria mbalimbali za mirathi zibadilishwe?, leteni mapendekezo yenu , hili ni jukumu letu sote, sisi tupo na hapa wizarani tunao wataalamu watazipitia na kuona namna ya kuzifanyia kazi, ili ziendane na wakati uliopo sasa, alisema na kuongeza kuwa ndio maana amesema Katiba Inayopendekezwa ina vipengele vingi ambavyo vitasaidia kuondoa uonevu kwa wanawake nchini itakapopitishwa na wananchi kupitia kura ya maoni.”

  KIKUHAMI chini ya Uongozi wa Bibi Thabita Siwale ulimuomba Waziiri wa Katiba na Sheria Dkt Mwakyembe kuangalia uwezekano wa kuondoa sheria zinazowakandamiza wanawake hasa zile za mirathi kwani zinawafanya wanawake hasa wajane kunyanyasika katika nchi yao.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: TUNAZISUBIRI NEC NA ZEC KUIPIGIA KURA YA MAONI KATIBA INAYOPENDEKEZWA Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top