728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Wednesday, July 27, 2016

  TAARIFA YA AJALI YA KICHWA CHA TRENI KUGONGANA NA BASI LA UDA JANA USIKU

  KAMPUNI YA RELI TANZANIA(TRL)

  MTU MMOJA AFARIKI KATIKA AJALI YA KICHWA
  TRENI KUGONGANA NA BASI LA UDA JANA USIKU

  Mtu mmoja afariki dunia baada ya  basi la UDA kukigonga kichwa cha treni cha Kampuni ya Reli Tanzania(TRL) katika  makutano ya reli na barabara ya Kamata saa 3:20 usiku jana Julai 26, 2016. Marehemu ametambuliwa  kwa jina la Omari Abdallah Nyumba  mkazi wa Mbagala.Aidha majeruhi 43 wa ajali hiyo walipelekwa hospitali ya Taifa ya Mhimbili ambapo watatu kati yao ni mahututi.
  .
  Taarifa za awali za Kikosi cha Polisi  Reli zinaeleza kuwa ajali  hiyo ilitokea baada ya dereva Majuto Hamis  wa basi hilo la UDA aina ya Hecher lenye namba za usajili T969 CVP kukaidi amri ya kusimama iliotolewa na Mfanyakazi  wa TRL. Dereva huyo ni mmoja wa majeruhi ambaye amevunjika miguu na yuko chini ya ulinzi wa Polisi wa Reli akiwa wodini baada ya majeruhi wote kupatiwa huduma.

   Kichwa cha treni kilichogongwa ni cha kazi za sogeza Namba 7317 kilikuwa  kikitokea  kituo kikuu cha treni cha  Dar es Salaam. 

  Kikosi cha Polisi TRL wameahidi kutoa taarifa zaidi baadae hii leo kuhusu maendeleo ya majeruhi wa ajali hiyo.

  Tokea uanze mwaka huu kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa wa sheria za barabarani kwa watumiaji wa vyombo vya moto hasa madereva wa pikipiki za bodaboda kutokuwa makini katika kuzitii sheria hizo zinazosimamia makutano ya reli na barabara. 

  Tokea kuanza kwa mwaka huu wa 2016 ajali nyingi zimeripotiwa hapa jijini Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Manyoni mkoani Singida zikihusisha vyombo hivyo.Wito unatolewa na Uongozi wa TRL kwa watumiaji wa vyombo vya moto boda boda , magari mkubwa na mabasi na wananchi kwa jumla kuzingatia sheria ili kuepuka madhara makubwa  ikiwemo kupoteza maisha, kupata ulemavu wa kudumu na pia upotevu wa rasilimali muhimu ambazo kama zikitumiwa vizuri zitaboresha maisha ya wananchi na Taifa  kwa ujumla.

  Imetolewa na Afisi ya Uhusiano:
   Kwa niaba ya  Mkurugenzi Mtendaji wa TRL 
  Ndugu Masanja Kungu Kadogosa
  Julai 27, 2016
  DAR ES SALAAM
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: TAARIFA YA AJALI YA KICHWA CHA TRENI KUGONGANA NA BASI LA UDA JANA USIKU Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top