728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Tuesday, July 12, 2016

  SMZ YAFANYA MAGEUZI YA VYETI VYA KUZALIWA

  Na Mwashungi Tahir -Maryam Kidiko. Maelezo Zanzibar. 

  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mageuzi ya vyeti vya kuzaliwa kutoka mfumo uliozoeleka wa kutumia karatasi pekee (PAPER BASED) kwenda katika mfumo wa kisasa unaotumia komputa.

  Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Habari Utalii na Michezo huko kikwajuni mjini Zanzibar.

  Amesema jitihada hizi zinalenga kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma kwa haraka na utunzaji mzuri wa kumbukumbu za usajili na kufanikisha upatikanaji wa takwimu za uhakika ambazo ni muhimu katika kuiwezesha Serikali kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.

  Aidha amefahamisha kuwa Serikali hiyo imeamua kuhamisha Ofisi ya Mrajis wa Vizazi , Vifo na Kadi za Utambulisho ambayo ndio yenye mamlaka kisheria kusajili matukio ya kijamii (vizazi , vifo ndoa na talaka) katika ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kwa madhumuni ya kuunganishwa usajili wa mtoto tangu kuzaliwa mpaka kufariki kwake.

  Hata hivyo ameeleza kuwa vyeti hivyo vinavyotolewa katika mfumo huo mpya vinamuonekano mzuri na ukubwa ukilinganisha na vile vilivyozoeleka ambavyo huchapwa kwa kutumia typewriter. Vile vile alisema kupitia mfumo huo muombaji wa cheti cha kuzaliwa hutakiwa kuwasilisha uthibitisho wa taarifa ya kizazi kutoka Hospitalini au kwa Sheha pamoja na taarifa nyengine ili kuingizwa katika komputa na kuweza kupatikanwa cheti kwa haraka.

  “Napenda kusisitiza kwamba utaratibu huu unafanyika kwa vizazi ambavyo taarifa zake zitakuwa zimeingizwa katika komputa na kwa vizazi ambavyo taarifa zake hazijaingizwa katika komputa utaratibu utakaoendelea kutumika ni uleule wa asili hadi ofisi itakapoweza kuingiza taarifa zote za vizazi katika mfumo mpya wa usajili .”Alisema waziri huyo.

  Sambamba na hayo aliwataka wananchi wote wa mkoa wa Mjini Maghribi Unguja watakapojaaliwa kupata watoto kufika katka ofisi husika iliopo Mazizini wakiwa na taarifa zote zinazohitajika na kusajili vizazi vyao katika mfumo mpya ulioanzishwa .

  Haji omar Kheir amesisitiza kuwa kila mtu ni haki yake kusajili vyeti hivyo kwa kufuata utaratibu maalum uliowekwa na ofisi hizo. Jumla ya Vyeti 480 vitaanza kutolewa rasmin hivi karibuni katika Mkoa mjini Magharibi.

  IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: SMZ YAFANYA MAGEUZI YA VYETI VYA KUZALIWA Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top