JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


PROFESA MUHONGO AAGIZA MAJI YA NYAMONGO KUPIMWA TENA.

Share This

  Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye koti la Bluu) akizungumza na wananchi katika kijiji cha Matongo wilayani Tarime. Profesa Muhongo alifika kijijini hapo ili kuwaeleza wananchi, maamuzi ya Serikali yanayotokana na mapendekezo  ya Kamati iliyoundwa mwezi Februari mwaka huu ili kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (kushoto),  akizungumza na wananchi katika kijiji cha Matongo wilayani Tarime) wakati  Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye koti la Bluu) alipofika kijijini hapo ili kuwaeleza wananchi, maamuzi ya Serikali yanayotokana na Mapendekezo ya  Kamati iliyoundwa mwezi Februari mwaka huu ili kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Baadhi ya wananchi katika kijiji cha Nyabichune wilayani Tarime, wakimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) aliyefika kijijini hapo ili kuwaeleza wananchi, maamuzi ya Serikali yanayotokana na Mapendekezo ya  Kamati iliyoundwa mwezi Februari mwaka huu ili kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje akisoma Ripoti kuhusu tathmini ya Mgogoro kati ya mgodi wa Acacia North Mara na Wananchi wanaozunguka mgodi huo. Ripoti hiyo aliisoma mbele ya  Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye koti la Bluu) aliyefika katika kijiji cha Matongo ili kuwaeleza wananchi, maamuzi ya Serikali yanayotokana na Mapendekezo ya  Kamati iliyoundwa mwezi Februari mwaka huu ili kutathmini migogoro kati mgodi wa Acacia NorthMara na wananchi wanaozunguka mgodi huo.

Na Teresia Mhagama.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ametoa agizo   la kupimwa tena kwa maji yanayotoka katika vyanzo vinavyozunguka mgodi wa dhahabu wa Acacia North Mara ili kujiridhisha kuwa hayana athari kwa binadamu, mifugo na mazingira.

Agizo hilo alilitoa wilayani Tarime wakati  akizungumza na wananchi katika vijiji vya Matongo, Nyabichune, Mrwambe na Nyakungulu ambavyo vinazunguka mgodi huo wa dhahabu.

Profesa Muhongo alitoa agizo hilo baada ya Kamati iliyokuwa ikitathmini migogoro kati ya Mgodi huo na wananchi kueleza kuwa matokeo ya vipimo vya  maabara vinaonyesha kuwa maji hayo yana viwango vinavyokubalika kwa matumizi ya binadamu, mifugo na mazingira na kupendekeza kuwa wataalam wa afya na mifugo wafanye utafiti zaidi ya suala hilo ili kujiridhisha zaidi.

“Viwango vinavyopaswa kutumika katika upimaji wa maji haya lazima viwe vya Shirika la Afya Duniani (WHO) hivyo zichukuliwe tena sampuli za maji wakati wa kiangazi na wakati wa mvua na zipimwe tena. Sampuli hizo zigaiwe kwa makundi mbalimbali ikiwemo wananchi, Mkuu wa wilaya, Kamati iliyofanya tathmini na mimi mwenyewe ili kila kundi lipeleke katika maabara inayoaminika na baadaye kuwasilisha majibu ya uchunguzi,” alisema Profesa Muhongo.

Aidha alisema kuwa sampuli za maji atakazopatiwa yeye  atazipeleka katika nchi  mbalimbali duniani ikiwemo Ujerumani na Ubelgiji ambako kuna maabara za kisasa na zinazoaminika duniani.
Aliongeza kuwa, vyanzo vya maji katika sehemu nyingi zenye uchimbaji mkubwa na mdogo duniani vimekuwa vikiathiriwa na shughuli za  migodi na kueleza kuwa atawasiliana na Mamlaka zinazosimamia Sekta ya Maji pamoja Mgodi ili kupata chanzo mbadala cha maji na hivyo kuondoa malalamiko ya wananchi wanaozunguka mgodi huo.

Aidha aliagiza wataalam wa Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha kuwa kila baada ya miezi mitatu wanachukua sampuli za maji  katika vyanzo vinavyozunguka mgodi huo na kuzipima ili kujiridhisha kuwa maji hayo hayana madhara kwa binadamu, mifugo na mazingira.
Naye Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche alimshukuru Waziri wa Nishati na Madini kwa kuamua kuishughulikia changamoto hiyo ya maji kwa kutoa agizo kuwa upimaji wa maji hayo uwe endelevu na  kutafuta chanzo mbadala cha maji.

Aidha Profesa Muhongo alitumia fursa hiyo kuwaasa Wachimbaji  wadogo kujiunga katika makundi ambayo yatawawezesha kufaidika na masuala mbalimbali  ikiwemo Ruzuku  inayotolewa na Serikali ambapo kwa mwaka huu, takribani Dola za Marekani milioni 400 zinatumika kuwaendeleza wachimbaji wadogo kupitia Ruzuku hiyo. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad