728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Friday, July 15, 2016

  MAKAMU WA RAIS KUHUDHURIA MKUTANO WA 27 WA WAKUU WA NCHI WANACHAMA WA UMOJA WA AFRIKA (AU) NCHINI RWANDA.

  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania SAMIA SULUHU HASSAN ataondoka nchini kesho Trh 17/07/2016 kwenda KIGALI nchini Rwanda kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa 27 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).

  Makamu wa Rais atamwakilisha Rais Dkt JOHN MAGUFULI katika Mkutano huo wa siku MBILI ambao unatarajiwa kufanyika KIGALI – RWANDA kuanzia Julai 17-18 mwaka huu.

  Katika Msafara wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania SAMIA SULUHU HASSAN atafuatana na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Kikanda na Kimataifa Balozi AUGUSTINE MAHIGA na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Zanzibar Issa Haji Ussi.

  Mkutano huo ambao utahudhuriwa na Makamu wa Rais utaanza kwa vikao vya ndani ambapo viongozi watajikita katika kujadili masuala ya kimkakati ikiwemo umuhimu wa kuliunganisha Bara la Afrika kibiashara kwa kuwa na soko la biashara huria ifikapo mwaka 2017 pamoja na mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

  Aidha Wajumbe wa mkutano huo wa 27 wa AU pia watachagua Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika pamoja na Makamu wake, Makamishna WANANE wa sekta mbalimbali na Majaji WANNE wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu pamoja na na kupitisha mapendekezo kuhusu gharama za uendeshaji wa umoja huo na bajeti ya fedha ya mwaka 2017.

  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania SAMIA SULUHU HASSAN na Ujumbe wake wanatarajia kurejea nchini Julai 19 mwaka huu baada ya kumalizika kwa Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) KIGALI nchini RWANDA.

  Imetolewa na
  Ofisi ya Makamu wa Rais.
  Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: MAKAMU WA RAIS KUHUDHURIA MKUTANO WA 27 WA WAKUU WA NCHI WANACHAMA WA UMOJA WA AFRIKA (AU) NCHINI RWANDA. Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top