728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Friday, July 29, 2016

  Dkt Kalemani aagiza ufuatiliaji makini sekta ya madini


  Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kushoto) akiwakabidhi viongozi wa Wilaya ya Sikonge, kifaa kinachotumika kuunganisha umeme pasipo kutumia nyaya za kawaida za kuunganishia kijulikanacho kitaalam kama ‘Ready Board’ au UMETA (Umeme Tayari), wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kiloleli wilayani humo hivi karibuni.
  Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (kushoto), akikagua mtambo unaotumika kusukuma maji kwa ajili ya matumizi ya wakazi wa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora hivi karibuni. Mtambo huo uliopo katika eneo la Utyatya, hutumia mafuta ya dizeli ambayo ni gharama kubwa. Eneo hilo ni mojawapo ya maeneo yanayotarajiwa kuunganishiwa umeme wa REA Awamu ya Tatu na hivyo kuondoa kabisa changamoto hiyo. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Peres Magiri.
  Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa huo, Thea Ntala akizungumza na wananchi wa eneo la Kiloleli wilayani Sikonge mkoani humo hivi karibuni wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani kukagua utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili.
  Mbunge wa Sikonge, George Kakunda (kushoto) akimweleza jambo Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (katikati), wakati wa ziara ya Naibu Waziri wilayani humo hivi karibuni kukagua utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Peres Magiri.


  Wananchi wa Kata ya Mole wilayani Sikonge, Mkoa wa Tabora, wakimpungia mikono Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani, ikiwa ni ishara ya kufurahishwa na yale aliyokuwa akiwaeleza wakati wa ziara yake kijijini hapo hivi karibuni.

  Na Veronica Simba – Sikonge


  Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani, ameagiza ufuatiliaji makini, hususan kwa wawekezaji wakubwa wa madini nchini wenye leseni za utafiti ili kujiridhisha endapo wanafuata kanuni na sheria husika.

  Dkt Kalemani alitoa agizo hilo hivi karibuni (Julai 27) kwa Afisa Madini Mkazi wa Tabora, Mhandisi Gasper Kachenge, alipokuwa katika ziara ya kazi wilayani Sikonge mkoani humo.

  Agizo hilo la Naibu Waziri lilitolewa kutokana na taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Madini, iliyowasilishwa kwake na Mhandisi Kachenge ambayo pamoja na mambo mengine ilieleza kuwa kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wawekezaji wakubwa wa madini wenye leseni za utafiti mkoani humo, kutoyafanyia kazi maeneo yao.

  Aidha, malalamiko hayo pia yalitolewa kwa nyakati tofauti mbele ya Naibu Waziri na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa huo, Thea Ntala pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Peres Magiri wakati wa ziara hiyo.

  Dkt Kalemani alimtaka Afisa Madini Tabora, pamoja na mambo mengine, kufuatilia na kuandaa ripoti endapo wamiliki wa leseni za utafutaji madini mkoani humo wanafuata taratibu na sheria ya madini ya mwaka 2010, inayowataka kuwasilisha taarifa za utafiti wao kila baada ya miezi mitatu.

  “Utuletee wizarani taarifa husika mapema iwezekanavyo ili tuchukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisisitiza Naibu Waziri.

  Naibu Waziri aliwataka maafisa madini kushirikiana na Halmashauri zote katika maeneo yao mkoani humo kwa kuandaa takwimu za wachimbaji wote wa madini ambazo zitabainisha mchimbaji yupi anapaswa kulipa kodi ipi ili Halmashauri ziweze kuwabana hususan katika malipo ya ushuru wa huduma (service levy) unaopaswa kulipwa kwao.

  Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ofisi yake kwa Naibu Waziri, Mhandisi Kachenge alisema kuwa jumla ya mrabaha wa shilingi milioni 29 umekusanywa kutokana na mauzo ya dhahabu katika eneo hilo hadi hivi sasa.

  Pia, akizungumzia mafanikio katika sekta ya madini mkoani humo, alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imetoa leseni nne kwa kikundi cha Tumaini Miners Group na leseni moja kwa Kikundi cha Umoja Miners Group ambapo zaidi ya wananchi 5000 wa maeneo ya Undomo, Mwanshina, Nhobola, Mbogwe na Lusu wamenufaika kwa kupata ajira kutokana na uwepo wa leseni hizo.

  Madini yanayopatikana na kuchimbwa katika Mkoa wa Tabora ni pamoja na dhahabu, vito, almasi, mawe ya chokaa na madini ya ujenzi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Dkt Kalemani aagiza ufuatiliaji makini sekta ya madini Rating: 5 Reviewed By: Ahmad Michuzi
  Scroll to Top