728x90 AdSpace


 • Habari za hivi Punde

  Tuesday, July 26, 2016

  Abu Dhabi yaendelea kujihimarisha katika kukuza sekta ya utalii, Uarabuni.


  Abu Dhabi. Kutokana na utamaduni uliojengeka kwa nchi za Falme za Kiarabu, uwapo wa vivutio na ukarimu kutoka kwa wenyeji ni mambo ambayo yameifanya Abu Dhabi kuwa sehemu muhimu kwa utalii.


  Milango imefunguliwa na watalii wanakwenda kujionea vivutio, huku wakiwa na uhakika wa kupata huduma nzuri za malazi, kujionea ukanda wa jangwa na huduma bora za hoteli.

  Miaka ya nyuma Abu Dhabi ilikuwa na baadhi ya vivutio na jangwa walikokuwa wanaishi makabila wazawa na nyumba zao za kiasili wakiwa wamezungukwa na vivutio vya kiasili.

  Uchumi wao ulitegemea zaidi uvuvi na kilimo cha chikichi. Pia, kulikuwa na nyumba zisizozidi 300 ambazo zilijengwa kiasili.

  Hivi sasa Abu Dhabi ambao ndio mji mkuu wa Nchi za Falme za Kiarabu umejiimarisha kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati na kuwa mji maarufu kwa utalii. Jambo hilo halikuwa rahisi kutokana na historia ya eneo hilo hususan kwenye utamaduni na vivutio vya asili.

  Kukua kwa kasi kwa jiji hilo ni kutokana na kutunza, kuhifadhi na kutangaza utamaduni wake wa kipekee na vivutio vya kale. Kwa maana hiyo imekuwa jambo rahisi kuhimarisha utajiri wa vivutio vya kale na sasa wageni wanaotembelea wameongezeka kujionea vivutio vya kitalii.

  Kuwapo kwa uvumbuzi wa mafuta katika eneo hilo, kumewezesha ukuaji wa mji huo kuwa wa kisasa zaidi na kuwavutia wageni kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni wakiwa na shauku ya kuona mambo ya kale na ya kisasa.

  Ni juhudi za kipekee za uongozi wa hususan Rais wa Falme za Kiarabu ambaye pia ni kiongozi wa Abu Dhabi, Mtukufu Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan kwa kuimarisha maendeleo ya miundombinu.

  Kwa kutambua mchango wa sekta ya mafuta, Abu Dhabi imekuwa ikipunguza kiwango cha uchafuzi wa mazingira ili kutoathiri shughuli za kiuchumi kwa wananchi wake.

  Mpango wa maendeleo wa Serikali wa mwaka 2030 ni kuwekeza kwenye utalii, usafirishaji, afya na elimu. Sekta ya utalii ndiyo inategemewa kwa kukuza uchumi wa nchi ikiwa ni matarajio ya kuhudumia wageni milioni 2.8 kwa mwaka na matarajio ya mwaka huu ni kuhudumia wageni milioni 2.

  Shirika la Maendeleo ya Elimu na Utamaduni Duniani UNESCO) limeitambua Abu Dhabi kuwa sehemu muhimu kwa vivutio vya asili na kiutamaduni kama vile uwapo wa jangwa, miamba, milima mirefu na chemchemi za tranguil, pwani yenye kilometa zaidi ya 400 na vitu ambavyo vimetengenezwa kuwavutia wageni.
  ​Vivutio.
  Mgeni awapo Abu Dhabi anaweza kujifunza mambo mbalimbali ya kiutamaduni na kuelewa mambo ya kale; historia na desturi za wenyeji. Wageni wanaweza kutembelea maeneo ya kale, ngome pamoja na msikiti mkubwa duniani, chemchem za kuvutia, kambi za jangwani, kuona wanyama kama ngamia.

  Sekta ya utalii nchini humo inaendeshwa kwa umakini na kusimamiwa na Mamlaka ya Utalii na Utamaduni Abu Dhabi (TCCA Abu Dhabi), ikiwamo kuendesha hoteli zenye hadhi ya juu ulimwenguni na nyumba ambazo zinakidhi matakwa ya wageni. Pia, inahakikisha waongozaji watalii wanafanya kazi yao kwa weledi na ufanisi kwa kila mgeni anavyopenda ahudumiwe.

  Abu Dhabi pia imekuwa mwenyeji mikutano mikubwa ya kimataifa kwa kuwa mwandaaji au mwanzilishi ikiratibiwa na TCA Abu Dhabi. Miongoni mwa mikutano hiyo ni iliyohusu watalii, chakula, matembezi ya familia, utamaduni na maonyesho ya sanaa.

  Familia ya Kifamle imekuwa madarakani Abu Dhabi tangu 1793, wamewezesha kuifanya jamii kuwa ya kisasa zaidi kwa kuimarisha heshima miongoni mwa jamii jambo ambalo limeweka msingi wa utamaduni waliorithi tangu awali.

  Kutokana na kuheshimu utamaduni wake, watu wa Falme za Kiarabu wamekuwa miongoni mwa jamii zenye utamaduni unaofahamika ulimwenguni jambo linalofanya kuwa sehemu muhimu kwa utalii.

  Ni mji miongoni mwa miji ya Falme za Kiarabu wenye idadi kubwa ya watu. Ongezeko la watu kwa sasa inakadiriwa kuwa milioni 2.3 na inaweza ikafikiwa watu milioni 3 kwa mwaka 2030.

  Hali ya hewa ya Abu Dhabi ni ya kitropiki. Hali ya mawingu na joto kwa kiwango cha juu huwa linajitokeza katika vipindi vya mwaka. Mvua hunyesha hasa kipindi cha baridi kati ya Novemba na Machi ikikadiriwa kipimo cha 12cms kwa mwaka.

  Mvua hunyesha hasa katika mji wa Oasis wa Al Ain ukiwa ni mji wa pili kwa ukubwa. Kutokana na mgandamizo wa hali ya hewa kwenye milima ya Hajal joto hukadiriwa kufikia 13c (50F) kipindi cha baridi hasa nyakati za usiku, na kiangazi hufikia 42C (118F) wakati wa usiku hufikia hadi 13C na 56F muda wa usiku.

  Wakazi wa Falme za Kiarabu ni takribani asilimia 20 tu ya jumla ya watu wote mjini humo kutokana na uwepo wa watu wengi kutoka mataifa mbalimbali.

  Dondoo kuhusu usafiri wa kuelekea Abu Dhabi
  ​Ndege aina ya Airbus A340-541 ya Shirika la Ndege la Etihad.

  Unaposafiri kuelekea Abu Dhabi, Shirika kuu la Ndege linalosifika kwa ubora ni "Etihad Airways" ambalo linatoa huduma bora na za kisasa. Shirika hilo ni la pili kwa ukubwa katika nchi za Falme ya Kiarabu nyuma ya Emirates,lenye makao makuu katika mji wa Khalifa, Abudhabi.

  Ni hivi karibuni tu Shirika hilo lilizundua safari za kila siku kati ya Dar es salaam na Abudhabi ambapo Shirika linatoa huduma kupitia ndege zake mbili ambazo ni Airbus A320 yenye nafasi 16 katika daraja la kwanza na daraja la kati nafasi 120. Huduma mpya imelenga kuwapa fursa wasafiri kwa safari za moja kwa moja kati ya Jiji la Dar es Salaam na Abu Dhabi.

  Dar es Salaam ni eneo ambalo watalii hufika ili kuweza kutembelea maeneo ya kitalii na kihistoria. Watalii wengi wa mataifa mbalimbali hufika kwa lengo la kutembelea maeneo ya kitalii ikiwamo Mlima Kilimanjaro, Mbuga ya Wanyama Serengeti na visiwa vya Zanzibar.

  Mji wa Abu Dhabi ni wa kwanza kwa ukubwa katika shirikisho la falme za Kiarabu kwenye rasi ya Uarabuni. Mwaka 2000 kulikuwa na wakazi zaidi ya 1,000,000. Mji huo mkubwa umejengwa kwenye kisiwa karibu na mwambao.

  Takriban 80% ya wakazi si wazalendo bali ni wageni. Mwaka 1970 ulikuwa ni mji mdogo uliokuwa umesheheni nyumba za matofali na matope.

  Lakini baada ya kupatikana kwa fedha za mafuta mji huo uliendelezwa kwa kasi na nyumba zote zilijengwa upya huku nyingi zikiwa ni za ghorofa.

  Maeneo ya Falme za Kiarabu pamoja na Qatar na Bahrain yalikuwa yanamilikiwa na makabila madogo na waliokuwa chini ya machifu wao.

  Tangu 1820 walikuwa na mikataba na Uingereza walipoahidi kuachana na uharamia na kushirikiana kiulinzi na Uingereza. Ulinzi huo ulizuia uvamizi wa Saudia katika karne ya 20.

  Falme hizo zilikuwa chini ya Uingereza hadi mwaka 1971, ambapo madola hayo madogo yalipata uhuru. Saba kati yake yaliungana kwa jina la Falme za Kiarabu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Post a Comment

  Item Reviewed: Abu Dhabi yaendelea kujihimarisha katika kukuza sekta ya utalii, Uarabuni. Rating: 5 Reviewed By: MICHUZI BLOG
  Scroll to Top