Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Prof Audax Mabula
akizungumza na waandishi wa habari,hawapo pichani.
Pichani kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Prof Audax
Mabula akizungumza na waandishi wa habari.
Pichani kushoto ni Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni
Bw Achiles Bufure, kushoto kwake ni Mratibu wa Onesho la Matumizi ya Ardhi na
Athari zake Bi Adelaide Salema pamoja na wanahabari mbalimbali wakimsikiliza
kwa makini Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho, hayupo pichani.
Pichani ni ni
mtafiti mzamivu katika
taaluma ya mazingira na matumizi bora ya ardhi kutoka Sweden Bi. Emma Li Johansson akizungumza na
waandishi wa habari. hawapo pichani.
Na mdau Sixmund
J. Begashe
Makumbusho ya
Taifa Tanzania kwa ushirikano na Chuo Kikuu cha Lund Sweden wameandaa onesho la
pamoja kuhusu mabadiliko ya matumizi ya ardhi katika bonde la Kilombero. Kwa
mara ya kwanza utafiti unatumia njia ya sanaa shirikishi katika kubainisha
madhara ya umilikishaji wa ardhi kwa wawekezaji wakubwa dhidi ya jamii ya
Tanzania.
Akizungumza na
waandishi wa Habari kwenye ukumbi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es
Salaam, Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa Prof Audax Mabula alitaja sababu ya
onesho hili la Umoja ni kutoa elimu kwa umma juu ya mabadiliko ya matumizi ya
ardhi ambayo kwa upande mwingine husababisha migogoro ndani ya jamii.
’’Afrika ni moja
ya maeneo ambayo yanahodhisha ardhi kwa gharama ndogo na kutoa malipo madogo kwa
wafanyakazi. Hata hivyo watafiti wengi wamekuwa wanalalamikia hali hii ya
umilikishaji holela ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa migogoro kwenye vyanzo
asili na kuleta ushindani na changamoto katika jamii za maeneo athirika’’
Alisema Prof Mabula.
Prof Mabula
aliongeza kuwa Watu wanayabadilisha mazingira hali ambayo huathiri watu na
maisha yao. Mabadiliko ya tabia nchi, kupungua kwa maji na ubora wake, kupungua
kwa mazalio ya samaki na wanyamapori, ongezeko la mifugo, vita baina ya
wafugaji na wakulima ni baadhi tu ya matatizo yanayosababishwa na binadamu.
Nae Bi.
Emma Li Johansson ambae ni mtafiti mzamivu katika taaluma ya mazingira na matumizi bora ya
ardhi amesema onesho hili ni matokeo ya utafiti alioufanya huko Kilombero
Mkoani Mprogoro kwa kutumia sanaa za maonesho kuruhusu watu kuelezea mtazamo
wao juu ya matumizi na mgawanyo wa ardhi katika maeneo ya vijijini mwao.
”Lengo ni kujua
namna vijiji vilivyobadilika tangu kukaribishwa kwa makampuni makubwa ya kilimo
ya kigeni ambayo yamehodhi ardhi kubwa kwa ajili ya kilimo cha kisasa. Sanaa
hii imetengenezwa kwa ushirikiano wa vijiji viwili athirika ambavyo vimeonesha
muonekano wake wakati uliopita, sasa na mpango maendeleo kwa wakati ujao.”
Alieleza Bi Emma
Akielezea program
ya onesho, Mratibu wa Onesho hilo Bi Adelaide Salema amesema kuwa, pamoja na onesho
hilo ,kutakuwa na mjadala kwa la lengo la kupaza sauti za wakulima wadogowadogo
na kukusanya hadhara ya wadau wa kada mbali mbali katika muktadha huu
kuzungumzia mabadiliko ya matumizi ardhi ili kuunda daraja baina yao na kuleta
ufumbuzi wa kadhia hii.
Onesho hilo litafunguliwa
rasmi tarehe 4 Machi 2016 saa tano kamili asubuhi na Bw. Jörgen Eriksson kutoka
ubalozi wa Sweden nchini Tanzania katika Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni iliyopo
Mtaa wa Shaaban Robert Kitalu Na. 6 mkabala na Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM)
na litadumu kwa muda wa mwezi mmoja tu
No comments:
Post a Comment