18/07/2012.
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema kuwa ugonjwa wa kansa na kifafa ni miongoni mwa magonjwa sugu yanayowasumbua wananchi wa rika zote na kwa uhakika ni kwamba tatizo hilo halijapatiwa ufumbuzi ulimwenguni kote.
Akijibu suala la Mwakilishi Mohammed Said Muhammed Jimbo la Mpendae aliyetaka kujua hatua gani unayochukuliwa na Serikali ya kupata tiba ya maradhi hayo pamoja na kufanya utafiti wa kina wa kuweza kujua asili na suluhisho la maradhi hayo .
Naibu waziri wa Afya Dk Sira Ubwa Mamboya alisema kuwa maradhi ya kansa na kifafa ni maradhi ya zamani na ni sugu ambayo yana sababu nyingi na zinazotofautiana . Alisema kuwa kwa hapa Zanzibar tuna madaktari ambao wanafanya kazi na kuchunguza na kuweza kutambua na wanapoweza kutoa tiba sahihi ya saratani na kifafa wanatoa ipasavyo kwa wagonjwa wa maradhi hayo .
Aidha alisema kuwa kutokana na sababu nyingi zinazojitokeza kwa maradhi hayo hata nchi zilizoendelea huwa zinataratibu zake za kuwa na wataalamu maalum ambao wanashungulikia tafiti tu za maradhi hayo na sababu nyingi za saratani na kifafa hazijaweza kujulikana vizuri hadi sasa “tatizo la maradhi hayo ni sugu na linachukuwa muda mrefu matibabu yake kila baada ya muda mgonjwa atahitaji kufanyiwa uchunguzi “alisema Dk Sira.
Dk sira alisema matibabu ambayo yanatolewa katika hospitali kuu ya mnazimmoja ni yale tu yanayowezekana kufanyika yasiyoweza kufanyika hapa wagonjwa hao hupelekwa nchi za nje kwa matibabu zaidi . Naibu huyo alisema kuwa wagonjwa huwa wanasafirishwa nchi za nje kutokana na kukosekana mashine za vipimo vya maradhi hayo serikali husafirisha wagonjwa hao kwa kufanyiwa matibabu lakini kuna baadhi ya wagonjwa ambao wanakuwa na haraka ya matibabu huamua kujigharamia wao wenyewe . Aidha alieleza kuwa wizara ya afya imeweza kufungua kitengo maalum ambacho kimetekwa kwa maradhi hayo ambayo yanaonekana ni sugu na ya muda mrefu .




Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment