Na Saida Ali na Salmin Juma, ZJMMC Zanzibar
Mkutano wa kimataifa wa Shirika la Kimataifa la mambo ya Bahari (IMO) umeanza leo Mjini Zanzibar ikiwa ni mara ya kwanza tangu Zanzibar kuwa mwanachama mshiriki wa IMO.Akifungua mkutano huo, Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu wa Zanzibar, Hamad Masoud Hamad alizitaka nchi zinazoshiriki kuhakikisha wanatunza mazingira ya bahari katika Mataifa yao.
“Mazingira yetu ya bahari mara nyingi yanaharibiwa na meli kubwa ambazo zinaharibu maeneo yanayolindwa kisheria, ni wajibu wetu kutunza usafi wa bahari” Alisema Waziri Hamad. Waziri huyo alisema azimio la namba A 982 linasisitiza haja ya kulinda maeneo maalum baharini ambayo yapo hatarini kuchafuliwa na shughuli mbalimbali za binadamu kama Meli kubwa kutupa taka karibu na fukwe za bahari.
Alisema kwamba pwani ya Afrika Mashariki nayo kama zilizvyo sehemu nyengine za bahari inamaeneo yanahitaji kulindwa kama yanavyoainishwa katika mpango wa PSSA. “Tanzania ina maeneo ya bahari ikiwemo ukanda wa bahari ya Pemba, kuzunguka kisiwa cha Mafia na Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa ambayo yanahitaji kuorodheshwa chini ya misingi ya PSSA.
Mbali ya bahari, Waziri Hamad aliuambia mkutano huo wa siku tano kwamba katika ukanda wa Afrika Mashariki pia kuna maziwa na mito ambayo yana maeneo yenye kuhitaji kulindwa na kuhifadhiwa kama ilivyo kwenye bahari. Alisema kumekuwa na ongezeko la meli za kimataifa ambazo zinahusika na utafutaji na uchimbaji wa mafuta katika biashara ya baharini hivyo ni jukumu la washiriki wa mkutano huo kutoa mikakati ya kulinda na kuhifadhi usafi wa bahari.
Mkutano huo umeandaliwa na IMO kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Majini Tanzania(SUMATRA) na Mamlaka ya Usafiri wa Bahari Zanzibar(ZMA). Jumla ya nchi 14 zinashiriki katika mkutano huo ambapo mada kuu ni kulinda rasilimali za bahari.



Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Post a Comment