Wednesday, December 29, 2010

JESHI LA POLISI LAWATUNUKU ASKARI WAKE VYETI VYA KUTUKUKA LEO JIJINI DAR.

Inspekta Jenerali wa Polisi Said Mwema pichani kulia akimpongeza meneja mauzo wa hsc Fatma Washoto (kushoto) jijini Dar leo,pichani kati akishuhudia ni Waziri wa Mambo ya Ndani Mh Shamsi Vuai Nahodha.

====== ======= ======== ======== ========


Benjamin Sawe na Mwanakombo Jumaa

Maelezo

Dar es Salaam


Jeshi la Polisi limewatunuku askari wake vyeti vya kutukuka na zawadi mbalimbali ikiwemo fedha taslimu kwa utendaji uliotukuka na raia walioshiriki kufanikisha utendaji wa kazi za polisi.

Akikabidhi zawadi hizo Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha amesema katika utekelezaji wa program ya maboresho, jeshi la polisi limebuni utaratibu wa kuwatunuku maafisa na askari waliotekeleza majukumu kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu.

Waziri Nahodha alisema utaratibu huo unaongeza motisha,ari na moyo wa kujituma kwa wale wanaotunukiwa na kupewa zawadi. “Nitawaunga mkono katika kutekeleza mambo yote yenye lengo la kuimarisha utendaji wa kazi zenu”Alisema Waziri Vuai.

Askari tisa na raia mmoja walikabidhiwa zawadi hati ya cheti cha ubunifu pamoja na pesa taslimu shilingi laki tano kila mmjoa kuhusu utendaji kazi wa kipolisi.Wengine waliokabidhiwa hati ya utendaji wenye uadilifu na uminifu ni askari nane na raia wawili ambapo askari hao walikataa rushwa ya shilingi milioni 17.

Kundi la tatu lililotunukiwa vyeti na pesa taslimu shilingi laki tano ni la maofisa wa polisi kumi ambao walifanikisha kutoa elimu ya polisi bara na visiwani. Wengine waliotunukiwa hati ya chetii ni askari elfu thelathini na nne waliokuwa katika madawati ya uchaguzi mkuu uliopita kumalizika kwa amani na utulivu.

Aidha askari 118 wa kanda maalumu ya Ilala walikabidhiwa vyeti vya sifa ambapo kikosi hicho kimekuwa kikipambana na majambazi na kati yao saba walitunukiwa vyeti vya sifa na zawadi. Wakati huohuo Waziri Vuai alizindua doria ya Jeshi la Polisi kwa kutumia baiskeli 30 ambao watakuwa wakizunguka katika kata mbalimbali ili kuimarisha usalama.

Akitoa maelezo kuhusu kikosi hicho Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Said Mwema alisema lengo la kuanzisha kikosi hicho ambacho kitashirikiana na raia ni kuongeza nguvu ya ulinzi kwa raia ambapo hatua hiyo ni moja kati ya maboresho ambayo yamefanywa na jeshi la polisi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.