Thursday, September 30, 2010

WAZIRI MASHA AWATAKA POLISI WASIVUNJike MOYO!

NA MAGRETH KINABO NA MARY KWEKA- MAELEZO

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Lawrence Masha amelitaka jeshi la polisi lisivunjike moyo kwa kuongezeka kwa taarifa za uhalifu katika vituo vya polisi bali wachukulie kama changamoto na kujidhatiti kukamirisha mikakati ya kukabiliana na matukio hayo.

Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri Masha wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya wakaguzi wasaidizi wa jeshi hilo, iliyofanyika katika Chuo cha Polisi Dar es Salaam. “Mnao wajibu wa kuwa mstari wa mbele katika kupanga mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizi,” alisema Waziri Masha.Alizitaja sababau za kuongezeka kwa matukio ya uhalifu kuwa ni maendeleo ya Sayansi na teknolojia, ukosefu wa ajira, utandawazi, umasikini, ukuaji wa miji, ongezeko la makazi holela, kuzagaa kwa silaha, imani za kishirikina,ongezeko la pengo baina ya matajiri na masikini pamoja na utumiaji na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Waziri Masha alisema kuongezeka kwa taarifa za uhalifu katika vituo vya polisi ni miongoni mwa mafanikio ya jitihada zinazofanywa na jeshi hilo, kuwahamasisha wananchi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu katika maeneo yao. Hata hivyo Waziri Masha aliongeza kuwa makosa yanayowakera wananchi kama unyanga’nyi na uvunjaji wa majumba na wizi yamepungua.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2008 makosa ya uvunjaji yalikuwa 27,491 na mwaka 2009 yalipungua hadi 26,561 hivyo kupungua kwa asilimia 3.4, wakati makosa ya wizi mwaka 2008 yalikuwa 31,130 na mwaka 2009 yalipungua hadi kufikia 28,427, hivyo yamepungua kwa asilimia 8.7.

Waziri Masha alilipongeza jeshi hilo, kwa kuendelea na mpango wa kuratibu na kusimamia mafunzo ya walinzi wa amani kimataifa ikiwa ni pamoja na kushiriki kwa vitendo shughuli za kulinda amani sehemu mbalimbali duniani.“Serikali inaendelea kuvijengea mazingira mazuri vyombo vya ulinzi na usalama na kutatua matatizo ya makazi na maslahi ya watumishi wake.

Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii(NSSF) katika mwaka huu wa fedha inaendelea na awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba za askari kwa kujenga maghorofa 30 kambi ya polisi barabara ya Kilwa, sita kambi ya Mabatini Mwanza, sita Musoma , Mara, Tatu Byekera ,Bukoba, 12 Ludewa Iringa, nane Kiwanja cha ndege Arusha, mbili Unguja Kuu Unguja na mbili Finya Kaskazini, Pemba.

Naye Mkuu wa chuo hicho, Elice Mapunda alisema kitaanza kutoa diploma ya sayansi ya polisi kuanzia mwaka 2010/2011 ikiwa ni jitihada za kukipandisha hadhi.Alisema jumla ya wanafuzi walioripoti katika mafunzo hayo walikuwa 356 na wote wamefaulu, lakini wawili kati yao walishindwa kushiriki kikamilifu baada ya kuumia wakiwa chuoni.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.