Wednesday, June 30, 2010

Bodi ya Biashara ya Nje imepiga marufuku maonyesho yote ya sanaa za Kitanzania ikiwemo ngoma, muziki na maigizo

Habari wa ndugu wapendwa.

Chama cha waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni Tanzania (CAJAtz) kimeshtushwa na kusikitishwa na uamuzi wa Bodi ya Biashara ya Nje (BET) wa kupiga marufuku maonyesho ya Muziki na Ngoma za Utamaduni katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam. Kupitia waraka wake uliotolewa na UTAWALA, BET imepiga marufuku maonyesho yote ya sanaa za Kitanzania ikiwemo ngoma, muziki na maigizo eti kwa madai kwamba yanaleta kelele.


Wakati huohuo muziki unasikika ni ule wa wasanii kutoka nje ya nchi kwenye maspika makubwa. CAJAtz inatambua thamani ya sanaa na Utamaduni wa Taifa hili na inaamini kwamba sehemu kama hizo ndiyo muafaka hasa katika kutangaza shughuli za sanaa na Utamaduni wetu.

Tunaamini pia kwamba katika maonyesho hayo ya biashara makampuni na asasi mbalimbali huwatumia wasanii katika kufikisha ujumbe wao kwa watu mbalimbali hasa kwa kuamini katika nguvu ya sanaa. lakini tunashangaa leo hii kuona BET inawataza wasanii kutumia fani zao kutoa ujumbe kwa watu licha ya kuwa makampuni na asasi hizo zimetumia pesa kuwakodi wasanii hao. CAJAtz inaamini kwamba sanaa ni biashara hivyo kwanza ilipaswa kuachwa ili ijitangaze kupitia maonyesho hayo. Pia BET inapaswa kufahamu kwamba kwa miaka yote ambayo wameilezeza kuwa na Mafanikio makubwa katika maonyesho hayo, sanaa na hizo ngoma zilikuwa zinatumika sana katika kusherehesha, kutoa ujumbe na kuelimisha wananchi juu ya mambo mbalimbali ya washiriki. Kwa kitendo cha kupiga marufuku maonyesho ya sanaa BET imekosa UZALENDO na utamaduni wetu na pia imebana ajira ya wasanii wengi walikuwa wameajiriwa na makampuni kwa ajili ya kufanya shughuli za maonyesho kwenye mabanda yao.

Kwa Msingi huo kama wadau wa masuala ya sanaa na Utamaduni hapa nchini, CAJAtz tunalaani vikali zuio hilo ambalo halina tija na limeegemea zaidi ulimbukeni na Kasumba ya watu wa kuthamini sanaa za nje na kuwatukuza wageni wachache kwa visingizio visivyo na maana. Iweje sanaa za Kitanzania iwe kelele na hizo za magharibi iwe burudani? Tunaiomba Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kulishughulikia suala hili haraka iwezekanavyo. Pia tunomba BET kutafakari upya zuio hilo.

Hassan Bumbuli
Katibu Mkuu CAJAtz

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.